Na Eleuteri Mangi, WUSM
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya michezo ambayo imewasilishwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo leo Oktoba 23, 2023 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kikao hicho na Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na uongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Husna Juma Sekiboko amesema kamati yake itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara hiyo ili kuhakikisha sekta ya michezo nchini inaendelea kupiga hatua na kuwanufaisha wananchi kiuchumi.
“Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipa kipaumbele sekta ya michezo tangu alipoingia madarakani, sote ni mashahidi, maono yake ni makubwa kwenye sekta hii” amesema Husna.
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro akijibu hoja mbalimbali zilizoulizwa na Wajumbe wa Kamati hiyo ukiwemo ukarabati unaoendelea wa Uwanja wa Benjamin Mkapa utakaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 31 hadi kukamilika kwake Agosti 2024, amesema kuwa ukarabati wa awamu ya kwanza ni asilimia 11 na umefanyika katika maeneo machache hatua iliyoruhusu kufanyika kwa ufunguzi wa michuano African Football League (AFL).
Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa ukarabati huo umewezesha kufanyika wa ufunguzi wa michuano hiyo Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam iliyoambatana na mchezo kati ya timu ya Simba ya Tanzania na Al Ahly ya Misri uliofuatiliwa na kutazamwa na wapenzi wa soka ndani na nje Tanzania pia kutumika katika mechi ya ligi hiyo kati ya TP Mazembe ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Esperance ya Tunisia uliofanyika Oktoba 21, 2023.
Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro amesema Serikali itajenga Uwanja wa Arusha ambao utakidhi vigezo vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na utatumika kwenye michuano ya AFCON 2027 kwa kuwa jiji la Arusha pamoja na sifa nyingine lina hoteli zaidi ya tano zenye hadhi ya nyota tano ambacho ni kigezo mojawapo cha nchi kupewa dhamana ya kuandaa mashindano hayo.
Waziri Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa Uwanja wa Dodoma utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 30,000 ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 234 kwamba inayoelekeza ujenzi wa uwanja wa michezo Makao Makuu ya nchi.
Viongozi wengine walioshiriki kikao hicho ni Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma, Katibu
Mkuu Bw. Gerson Msigwa, Menejimenti ya Wizara pamoja na Wataalam wa Wizara hiyo.