Rais Jakaya Kikwete, ameelezea kustushwa na kusikitishwa na vifo vya wasanii maarufu nchini, Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ na John Stephano Maganga.

Wasanii hao wa uigizaji, filamu, muziki na tamthilia walikufa katika kipindi cha wiki moja inayoishia Jumatatu wiki iliyopita. Wakati Sharo Milionea alikufa katika ajali, Mlopelo na Maganga walikufa baadaa ya kuugua.


Sharo Milionea alikufa wakati gari alilokuwa akiendesha kuelekea kwa mama yake wilayani Muheza, Tanga, lilipopinduka, Jumatatu wiki iliyopita.


Rais Kikwete amesema vifo vya wasanii hao ni pigo kubwa kwa Taifa kwani wameacha pengo kubwa katika tasnia ya sanaa ambako wamekuwa wakitoa michango mikubwa.


“Nimepokea kwa mshituko na huzuni kubwa habari za vifo vya wasanii hawa waliokuwa na michango mikubwa katika filimu na muziki… wameacha pengo kubwa ambalo kamwe alitazibika kwa muda mfupi,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi kwa familia za wasanii hao.