Na Mwandishi wetu Jamhuri Media Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Oktoba 18, 2023 amezindua zoezi la ugawaji vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi Mkoani humo, Uzinduzi ambao umefanyika Katika ukumbi wa Hoteli ya Lamada Ilala Boma.
Akiongea wakati wa Uzinduzi huo Chalamila amesema Serikali chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt Samia imekua ikitekeleza afua mbalimbali za Afya kwa lengo la kulinda Afya za Jamii na ustawi wao, moja ya maeneo yanayotiliwa mkazo ni udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza hususani ugonjwa wa malaria.
Ndio maana Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais- TAMISEMI na wadau wa maendeleo katika kukabiliana na magonjwa hayo imepanga kutekeleza kampeni za ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi ndani ya Mkoa zoezi ambalo nimezindua leo
Aidha Chalamila amesema kutokana na juhudi mbalimbali na mwitiko kwa wakazi wa Mkoa maambukizi ya malaria yamepungua sana kutoka wastani wa asilimia 6 miaka kumi iliyopita hadi asilimia 0.7 mwaka 2023, Mkoa wa DSM ni moja kati ya mikoa 9 ya Tanzania Bara yenye maambukizi kidogo, pamoja na mafanikio hayo malaria bado ni tatizo kwani mwaka 2022 wakazi 102 waliugua malaria kati yao 14 walithibitika kufariki baada ya kuugua.
Hivyo niwatake viongozi kuendelea kuongeza uelewa kwa jamii na katika taasisi mnazotoka ili wananchi wavipokee na kuvitumia kwa usahihi kila wakati vyandarua hivi ili kujikinga na Mbu waambukizao malaria, vyandarua hivyo vina ukubwa wa futi 5 kwa 6 ambavyo vinatosha kwenye malazi ya walio wengi pia vina viwatilifu vya muda mrefu vinavyoua Mbu, vimethibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu, vimetengenezwa hapahapa nchini.
“Niwaombe kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya malaria kama wataalam wanavyoelimisha ikiwemo kufukia madimbwi pamoja na kuwa tumegawa vyandarua” Alisema Chalamila
Kwa upande wa Mratibu wa Malaria Mkoa Dkt Ford wakati akitoa takwimu za kitaalam za hali halisi ya ugonjwa wa Malaria amesema maeneo ambayo yana kiwango kikubwa cha Malaria ni Luhanga Wilaya ya Ilala na Tudwi Songani kwenye maeneo hayo kati ya watu 100 wanaopimwa malaria zaidi ya 30 huthibitika kuwa na malaria.