Ni jambo zuri kuona na kusikia Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umetoa maazimio ya kukiimarisha chama hicho tawala na kushughulikia changamoto mbalimbali nchini.
Lakini hebu nithubutu kusema wazi kwamba mkutano huo uliofanyika kwa mbwembwe nyingi mjini Dodoma hivi karibuni, umetuhadaa. Katika baadhi ya maazimio yake umetuhadaa mchana kweupe.
Ninakiri kwamba yapo maazimio machache yanayotia matumaini. Mojawapo ni lile linalohusu mapambano dhidi ya rushwa, ambapo mkutano huo umeiagiza Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa chama hicho waliotoa rushwa wakati wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutengua matokeo ya ushindi wao.
Sasa tunasubiri kuona na kusikia kitanzi hicho kitamwangukia nani na lini hasa! Kwa ukweli usiopingika, baadhi ya maazimio yakiwamo yanayohusu usambazaji huduma za jamii kwa wote, kuboresha maslahi ya wakulima na wafanyakazi, kushughulikia mmomonyoko wa maadili, nidhamu, matumizi mabaya ya madaraka na uwajibikaji duni wa viongozi.
Ukisoma kwa makini maazimio hayo utabaini Mkutano Mkuu huo wa CCM umetuhadaa kwamba serikali itayatafutia ufumbuzi thabiti, lakini maneno uliyotumia ni butu, hayana makali yanayotoa msukumo kwa wahusika kuyatekeleza kwa vitendo.
Kusambaza huduma za jamii kwa wote
Mkutano Mkuu huo wa CCM umebainisha vipengele vya azimio hilo kuwa ni elimu, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, huduma za afya, maji na umeme.
Mkutano huo umeiagiza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuangalia uwezekano wa kuanza mchakato wa kuifanya elimu ya sekondari kuwa haki ya msingi kwa kila mtoto nchini.
Hapo tunaona namna mkutano huo wenye wajumbe zaidi ya 2,000 ulivyojichanganya katika azimio hilo. Umesema umeiagiza serikali lakini wakati huo huo umeiomba iangalie uwezekano wa kulitekeleza. Sitaki kuamini kuwa mkutano huo haujui kuwa kuagiza na kuomba ni vitu viwili tofauti. Hiyo ni hila tu!
Nimeendelea kujiuliza kwamba kulikuwa na ugumu gani kwa mkutano huo kutamka kitu kimoja kama ni kuiagiza au kuiomba serikali itekeleza azimio hilo? Imeanza kwa kuiagiza ikamalizia kwa kuiomba serikali iangalie uwezekano. Hapo ni wazi kuwa kitakachofanyiwa kazi ni neno la mwisho, kuangalia uwezekano. Mwisho wa siku serikali itajitetea kuwa uwezekano wa kutekeleza azimio hilo ulishindikana!
Kama Mkutano Mkuu wa CCM ungeiagiza badala ya kuiomba serikali kuangalia uwezekano, utekelezaji wa azimio hilo ungefanyika sambamba na kuboresha elimu ya msingi na sekondari kwa kukabili matatizo ya upungufu wa walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, madawati, vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za walimu. Pia kudhibiti gharama kubwa na michango holela shuleni. Elimu ingeboreshwa nchini.
Lakini pia, mkutano huo haukutamka ni hatua gani za kisheria na kinidhamu zinastahili kuchukuliwa dhidi ya viongozi wa idara husika iwapo watashindwa kutekeleza azimio hilo. Hili ni pungufu kubwa.
Kwa sababu hiyo, hata utaratibu wa sasa ambao mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu unategemea bajeti ya serikali huenda hautaboreshwa kuwezesha wanafunzi wote wenye sifa wanaoihitaji kuipata.
Vilevile, mkutano huo wa CCM haukutaja adhabu inayostahili kwa viongozi watakaoshindwa kusimamia utoaji wa huduma bora za afya, maji na umeme kwa wananchi vijijini na mijini. Maazimio yasiyotaja adhabu kwa watakaokaidi ni sawa na sifuri. Hii ni hadaa!
Kuboresha maslahi ya wakulima, wafanyakazi
Mkutano Mkuu huo wa CCM umeiagiza serikali iboreshe maslahi ya makundi hayo kwa kuyaongezea kipato kinachokidhi mazingira na gharama za maisha ya sasa, lakini cha ajabu umemalizia kwa kusema jambo hilo litekelezwe pale tu inapowezekana!
Hapo ni dhahiri hakuna kitakachotekelezwa. Maana serikali haikuagizwa bali uimeombwa kuangalia kama itawezekana kulitekeleza azimio hilo. Siku ya siku itajitetea kuwa matatizo ya wakulima na wafanyakazi yalikuwa juu ya uwezo wetu wa kiuchumi.
Hilo sasa si agizo, ni ombi tu kwa serikali. Sote tunajua kawaida ya ombi, linaweza kukubaliwa au kukataliwa. Hapo pia tunaona kwamba mkutano huo haukutaja adhabu itakayotolewa kwa wahusika watakaokaidi agizo hilo. Serikali iliyopo inaundwa na CCM, lakini chama hicho tawala mara nyingi kimekuwa kikikosa ujasiri wa kuisimamia kuhakikisha inashughulikia matatizo ya Watanzania kwa uzito unaostahili. Tatizo hapo ni nini hasa?
Matumizi mabaya ya madaraka
Licha ya Mkutano Mkuu huo wa CCM kukiri kutambua kuwapo kwa mmomonyoko mkubwa wa maadili, nidhamu, matumizi mabaya ya madaraka na uwajibikaji duni wa viongozi, bado umepata kigugumizi cha kutamka adhabu inayostahili kwa wanaokiuka misingi ya maadili ya uongozi na utumishi wa umma.
Mkutano huo umeishia kuihimiza serikali (inayoundwa na baadhi viongozi wasiyo waadilifu) ichukue hatua kali haraka dhidi ya viongozi waliomomonyoka kimaadili. Haukutaja aina ya hatua hizo na zichukuliwe haraka kwa muda gani.
Ndio maana ninasema CCM kimekabidhiwa madaraka ya nchi hii kwa muda mrefu lakini sasa kinaelekea kushindwa kuyatumia ipasavyo. Sasa kimefikia hatua ya kuuhadaa umma katika maazimio yake. Tusubiri hatima yake.