Na Allan Vicent, JamhuriMedia,Tabora
Kampuni ya Mbolea nchini (TFC) inatarajia kusambaza zaidi ya tani 75,000 za mbolea ya ruzuku iliyotolewa na serikali ya awamu ya 6 kwa wakulima zaidi ya 150,000.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Samwel Mshote alipokuwa akiongea na gazeti hili jana kwenye maonesho ya siku ya mbolea duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Chipukizi mjini Tabora.
Alisema mafanikio hayo yamechochewa na dhamira njema ya Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta ya kilimo ili kuwainua kiuchumi wakulima.
Mshote alibainisha kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 serikali imewatengea kiasi cha sh bil 40 kwa ajili ya kufanikisha mpango huo na kiasi kingine cha sh bil 70 kitatolewa na wadau wa maendeleo (wahisani).
Alifafanua kuwa tani 25,000 za awali tayari zimenunuliwa na kuanza kusambazwa kwa wakulima na sasa wapo kwenye mchakato wa kununua tani zingine 50,000 ambazo zitasambazwa katika Mikoa yote.
‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuiwezesha TFC kununua na kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini,’ alisema.
Mkurugenzi alibainisha kuwa awali kampuni hiyo ilisimama kwa miaka 8 kutokana na sababu mbalimbali lakini sasa baada ya kuwezeshwa imeanza kwa kasi kubwa ili kuhakikisha mbolea inayotolewa na serikali inawafikia walengwa wote.
Alisisitiza kuwa dhamira ya Kampuni hiyo ni kuboresha utendaji wake katika kuhudumia wakulima ili kuwa ya kwanza miongoni mwa kampuni zote za ununuzi na usambazaji mbolea nchini.
Mshote aliongeza kuwa baada ya kuanza tena shughuli zao mwaka jana; 2022/2023; serikali iliwapatia kiasi cha sh bil 6 ambapo walinunua na kusambaza tani 4,500 za mbolea hiyo na hadi sasa wameshahudumia zaidi ya wakulima 30,000 na kufikisha huduma hiyo katika Mikoa 17 ya Tanzania Bara na halmashauri 40.
Alieleza mikakati yao kuwa ni kununua na kusambaza zaidi ya tani 150;000 kuanzia msimu huu na kufikia wakulima zaidi ya laki 5.
Aidha aliongeza kuwa tayari wamesajili mawakala wa ununuzi na usambazaji mbolea wapatao 300 pia watatumia vyama vikuu vya ushirika na maghala ya serikali kuuza mbolea hiyo.
Mshote alitoa wito kwa wakulima kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kujisajili katika daftari huku akiwataka mawakala na wakulima wote kufuata taratibu za ununuzi wa mbolea hiyo ili wasiingie kwenye shida au kupata hasara.