Leo nchi yetu ina vyama vingi, lakini cha kufurahisha kwangu mimi ni kuwa karibu viongozi wote wa vyama vya siasa wamehenya katika kambi za JKT kwa mujibu wa sheria. Ebu angalia hapa, Mwalimu Nyerere (Operesheni Mwenge Mafinga- siku moja), Rais Jakaya Kikwete (Operesheni Tumaini – Ruvu kwa Mujibu wa Sheria), Benjamin Mkapa (Operesheni Tekeleza Ruvu – Mature Age).

Hawa wote ni wenyeviti wa CCM na wamekuwa marais wa nchi yetu. Kwa upande wa mawaziri wakuu, Rashid Kawawa (Operesheni Kazi B Ruvu – Mature Age), Edward Sokoine (Kazi B Ruvu -Mature Age), Frederick Sumaye (Operesheni Mwangaza Mafinga -Mujibu wa Sheria), Edward Lowassa (Operesheni Ukombozi, Mafinga- Mujibu wa Sheria), Mizengo Pinda (Operesheni Vitendo, Oljoro -Mujibu wa Sheria).


Hawa wote ni wa chama tawala. Lakini wa vyama vya upinzani nao wamepikika katika kambi za JKT. Angalia hawa, John Cheyo – UDP (Operesheni Kilimo, Mafinga – Mujibu wa Sheria), Profesa Ibrahim Lipumba – CUF (Operesheni Jikomboe, Ruvu -Mujibu wa Sheria), Mabere Marando – Chadema (Operesheni Jikomboe, Ruvu), Peter Mziray (Oljoro- Mujibu wa Sheria), Dk. Sengondo Mvungi -NCCR – Mageuzi (Oljoro -Mujibu wa Sheria).


Waheshimiwa wote hawa wamepikwa na wakapikika katika chungu kile kile cha JKT na wakajengeka kizalendo, ndiyo sababu wote hawa wanaelezea uchungu wao kwa nchi yao kwa mitazamo ya itikadi zao.


Wote wanakubali kuwa JKT ni chombo cha kujenga Umoja na Uzalendo wa Taifa. Lakini viongozi hawa wanatofautiana sana namna au njia za kutumia rasilimali za Taifa katika ujenzi wa Taifa. Kwa sababu hiyo, baada ya Baba wa Taifa kuhutubia waandamanaji pale Lumumba mnamo Oktoba 23, 1966 hotuba yake iliitwa “TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO” (kimepigwa chapa na Government Printer Dar es Salaam 1966).


Tujiulize hapa hawa wenye moyo ni akina nani? Kwa kweli ndiyo hao wabunge wanaoomba wapewe fursa za kuingia katika makambi ya JKT angalau wakae kwa muda unaokubalika. Lengo lao kubwa ni kushiriki katika kujenga Taifa hili wakisaidia kukomaza Umoja, Ushirikiano na Moyo wa Uzalendo kwa Taifa lao.


Kule kuathirika kiuchumi kwa Taifa letu kati ya miaka ya 1979 – 1993 kulilazimisha Serikali kusitisha kuita vijana wa mujibu kwenda kambini kuhudumia Taifa.


Lakini kwa jitihada na nguvu mpya ya Serikali imeweza kurejesha tena utaratibu wa kuweka vijana katika kambi za JKT kuanza mwaka 2002 kwa utaratibu wa kujitolea.


Lakini kutokana na ukereketwa wa wabunge vijana kutamani utaratibu wa kuwaita vijana wa mujibu wa sheria waingizwe kambini kutoa huduma kwa Taifa hili, ndipo sasa Taifa limeafiki nao waingie. Huu ni moyo wa uzalendo na ujasiri mkubwa. Ni wazi wananchi wameona ombwe lililoko katika ujenzi wa Taifa letu ambalo miaka ya nyuma liliheshimika sana kwa utayari wake katika ulinzi na ujenzi wake.


Labda hapa nirejee maneno ya Zitto Kabwe – Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) katika Bunge la 10 la Bajeti Dodoma namnukuu, “…Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya JKT kusimamishwa mwaka 1994 hapa katikati kumekuwa na vijana wengi sana wamemaliza kidato cha sita, wanamaliza vyuo vikuu na hawaendi JKT.

 

Baadhi ya vijana hao, mimi nikiwemo… hatujapitia JKT. Mheshimiwa Naibu Spika nilikuwa naomba nitoe rai, nilisema hili mwaka 2006 halijafanyiwa kazi naomba lirejewe kwamba vijana wote ambao ni viongozi wa kisiasa ambao hatukupita JKT tuandaliwe mafunzo maalumu ya JKT kuanzia sasa…” (Tazama VIJANA LEO toleo maalumu la Novemba 2011 uk. 6 – 7).


Mheshimiwa Kabwe alikwenda mbali zaidi pale alipoomba mchakato huo uharakishwe kwa mafunzo ya wiki nane kuanzia mwishoni mwa Bunge lile. Akasema hiyo itakuwa kama kichocheo (motisha) kwa vijana wengine kujiunga JKT.


Alielezea umuhimu wa JKT kwamba wazee wao (yaani waasisi wa utaratibu huu wa National Service) waliwajengea misingi imara ya kuwatumikia wananchi, uwajibikaji, nidhamu na kuondoa tofauti zilizojitokeza katika Taifa hili.


Waziri wa Ulinzi na JKT wakati ule, Dk. Hussein Mwinyi, alilikubali ombi lile kwa kuwahakikishia wabunge kuwa ombi lao limepokewa na kuwa utaratibu unaandaliwa kurejesha mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.


Akafafanua kuwa Taifa lilikuwa na vijana takribani 36,000 wanaohitimu kidato cha sita kila mwaka na utaratibu utakapokamilika mwaka wa fedha wa 2012/2013 utatekelezeka. Jambo hili ameliona limevuta hisia za watu wengi ndani na nje ya Bunge.


Kuonesha utayari wa JKT kuwaita vijana wa mujibu wa sheria, Mkuu wa JKT wakati ule Meja Jenerali Samuel Kitundu, alisema namnukuu, “… Tumepokea ombi hilo kwa moyo wa dhati na sasa tunafanya maandalizi katika makambi yetu ili kuweza kutoa mafunzo stahili kwa waheshimiwa wabunge wetu. Wabunge vijana wameonesha moyo wa kizalendo kwa kutambua umuhimu wa JKT kuwa mojawapo ya taasisi zilizojenga uzalendo na umoja wa Taifa letu”.


Akaainisha kambi za Ruvu (Pwani) na Oljoro (Arusha) zinaandaliwa kutoa mafunzo kwa waheshimiwa wabunge hao. Aidha, JKT inaandaa wakufunzi wa kutosha watakaoweza kutoa mafunzo yanayokidhi matakwa ya nchi; na programu maalumu inaandaliwa kuwawezesha wabunge kujifunza mafunzo ya kijeshi, nidhamu na stadi sawa na vijana wengine wanaojiunga JKT.


Kwa mtazamo namna hii wa waheshimiwa wabunge vijana wenye ari, moyo na nia thabiti ya kujenga Taifa hili, ninaamini kabisa Taifa linaelekea katika uelewano, mshikamano na utaifa wenye uzalendo thabiti. Vijana katika Bunge wana itikadi zao tofauti kabisa, lakini wameona umuhimu wa kushirikiana katika kulijenga Taifa hili ambalo siku za hivi karibuni limeonesha kutambiana, kubezana, kuvutana kila watu upande wao ambavyo ni kulimega Taifa katika matabaka.


Ni lazima Serikali na sisi wananchi wote tuwapongeze vijana hawa kwa kutuonesha njia sahihi ya kujenga Taifa hili. Ndiyo sababu nilisema hapo awali ndugu yangu Charles Charles anaposema JKT ya wiki tatu ni utani hakuwa sahihi. Alitoa mtazamo wake yeye baada ya kuhenya kule Msange na Kunduchi RTS akajua hee hawa jamaa wanakuja kufanya danganya toto! Mzatamo namna ile mimi nauita hasi (pessimistic).


Tunatakiwa Watanzania wote tuwe na mtazamo chanya (optimistic). Vijana wa mujibu wa sheria wana nafasi nzuri katika CTS kuleta mageuzi ya haraka katika kushikamana pamoja na kuzalisha mali kitaalamu zaidi.

ITAENDELEA


Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).