Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedua, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita inayooongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, imelenga kubadilisha fikra, mitazamo na utendaji wa wataalamu ngazi ya Msingi ili wananchi wawe kitovu cha maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju wakati wa kufunga Mafunzo ya Siku Mbili kwa Wataalam wa Ngazi ya Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na tarafa zake tano, Kata 36 na Vijiji 106, yaliyohusu kuwapitisha kwenye Mpango wa Taifa wa Uhamasishaji na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa 2022/2023 hadi 2025/2026.
Amesema nia ya Serikali ni kuwawezesha wananchi kueleza matokeo ya huduma za kijamii, miundombinu na maendeleo wanayopelekewa na Serikali huku akisisitiza kuwa Jamii ndiyo iwe chachu ya kuhimiza maadili, kuendeleza ulinzi na uendelevu wa rasilimali na hata usalama.
“Kila Kata ikamilishe na kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa Mpango kwa kuwa, mafunzo bila ya kuwa na mipango kazi ya utekelezaji ni upotezaji wa rasilimali fedha na muda, ni wajibu wenu kuweka utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu. Mjenge mazoea ya kufanya kazi kwa timu na kuwajibika ili kuwa na kazi zenye matokeo na tija.” amehimiza Mpanju.
“Serikali inatambua mchango wa Timu ya Wataalam Ngazi ya Kata katika kutoa huduma kwenye nyanja mbalimbali na utaalam kwa jamii. Mtambue ya kuwa Serikali inawategemea sana katika kuchangia maendeleo ya Taifa. Nawapongeza kwa kazi nzuri, Kazi iendelee,” amesema Mpanju.
Naibu Katibu Mkuu Mpanju pia ametumia mkutano huo kulishukuru shirika la Save the Children kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kutoa huduma kwa wanachi na kuimarisha utendaji wa wataalamu wake, amehitimisha kuwa ushirikiano huu umekuwa mwazo mzuri unaoonesha ishara ya mafaniko kwa siku zijazo.