Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri. Baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri wamepoteza nafasi walizokuwa wakishikilia, kutokana na kashfa ya ufujaji wa fedha na mali nyingine za umma.
Sakata lote lilianza baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kutoa ripoti iliyosheheni kila aina ya uozo katika wizara, idara na taasisi mbalimbali za umma.

Kwa ufupi ni kwamba fedha zilizotafunwa na baadhi ya watendaji ni nyingi mno. Baadhi ya mawaziri – ama wao wenyewe au wasaidizi wao – wamejikuta wizara zao zikikabiliwa na kashfa kubwa ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuwapa fursa wabunge kujadili ripoti ya CAG, ambayo hatimaye imeibua mabadiliko haya makubwa. Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa Baraza la Mawaziri, wale walioteuliwa walianza kujipongeza.

Wapo waliowaalika ndugu, jamaa na marafiki zao kwa ajili ya kujipongeza. Kweli, ni kawaida kwa binadamu kuonyesha furaha kutokana na mafanikio anayoyapata, lakini sisi hatuamini kama kweli ni busara kwa mawaziri na naibu mawaziri kujiandalia sherehe kujipongeza.

Kuteuliwa kwao kulitosha kuwafanya wajiinamie, watoe machozi na wajipime kama kweli wanaweza kutimiza kile kinachotarajiwa na aliyewateua, na zaidi ya wote, Watanzania walio na kiu ya kuona mabadiliko ya kweli.

Kuandaa sherehe kunaweza kutafsiriwa kuwa walichokuwa wakikisubiri sana ni kuteuliwa kuwa mawaziri au naibu mawaziri, na si dalili ya kuonyesha kuwa wana kiu na dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania.

Tunatoa wito kwa mawaziri na naibu mawaziri wote kutambua kuwa Watanzania wana kiu ya kuona mabadiliko. Wana hamu ya kuwaona wakisimamia wizara, idara na taasisi zao kwa weledi wa hali ya juu na kwa nguvu zao zote.

Kama yupo waziri anadhani kwamba kwa kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo ndiyo mwanzo wa kumaliza umasikini wake wa kipato, huyo anajidanganya.

Somo lililowapata wenzao walioondolewa kwenye nafasi zao ni kubwa na zito. Waswahili walisema ‘Ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji’. Wasidhani kuwa wao watadumu kwa miaka yote katika nafasi hizo.

Kwa wizara kama ya Maliasili na Utalii, waziri na naibu waziri wapya wanapaswa kuzitambua changamoto zinazoikabili wizara hiyo na kuhakikisha kuwa wanawatendea haki Watanzania.

Kwa sasa zipo juhudi za makusudi kabisa za mawakala wa wageni kutoka nje, wanaohangaika usiku na mchana wakitaka kuona kuwa kampuni za Wazungu zilizokosa vitalu zinavipata. Haya yako wazi kabisa.

Kusimamia sheria, kanuni na kuongeza uwazi katika wizara hiyo ndiyo salama yao. Kinyume cha hivyo watambua kuwa hawatadumu. Tangu mwaka 2005, sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa na mawaziri watano. Hii si kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na wanaoteuliwa kuiongoza kujisahau na kutopea kwenye ukwasi.

Tunawapongeza mawaziri na naibu mawaziri wote kwa kuteuliwa kwao, lakini watambue kuwa huu si muda wa kujiandalia sherehe, bali ni wa kutafakari kuona namna gani watakidhi kiu ya Watanzania ya kuwaletea maendeleo.