Na Steven Augustino,JamhuriMedia,Tunduru
WATU watatu wakazi wa vijiji vya Matekwe,Wilaya ya Nachingwea,mkoani Lindi na Tinginya Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma,wamefariki dunia katika mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyozuka katika maeneo hayo.
Kufutia hali hiyo diwani wa Kata ya Tinginya Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma aliyetambulika kwa jina la Aliasa Mshamu anashikiliwa na Polisi akituhumiwa kuhusishwa na mapigano yaliyoibuka kati ya wafugaji na wakulima.
Taarifa kutoka katika vijiji hivyo ambazo pia zimethibitishwa na mamlaka husika ya ulinzi na usalama,zinaeleza kuwa vurugu hizo zilitokea Septemba 23, mwaka huu majira ya mchana katika maeneo hayo.
Marehemu hao wametambuliwa kwa majina ya Kidabelega Longoda (31), Nyerere Kisingwenga (80) ambao ni wafugaji waliopangiwa kuishi na kufanya shughuli za kufuga katika Kijiji cha Matekwe,Wilaya ya Nachingwea, Mkoani Lindi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mtu mwingine aliyepoteza maisha katika tukio hilo ametambulika kwa jina la Fadhili Abdallah (33), mkulima mkazi wa Kijiji cha Tinginya katika Wilaya ya Tunduru,Mkoa wa Ruvuma anayedaiwa kushambuliwa na wafugaji kabla ya tukio la wao pia kwenda kushambuliwa.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda ambao waliomba majina yao kutotajwa kwenye vyombo vya habari, wametaja chanzo kuwa ni wafugaji kupeleka mifugo yao kulisha mazao shambani kwa marehemu Fadhili Abdallah.
Mashuhuda hao wameeleza kwamba baada ya tukio hilo mkulima huyo alipohoji sababu za wafugaji kulisha ng’ombe kwenye shamba lake,alijibiwa kwa kupewa kipigo kisha kupoteza uhai,hali iliyoibua hasira kwa wananchi wengine na kwenda kujibu mashambulizi kwa wale wafugaji.
Wamesema baada ya wanakijiji kuona mwenzao amepigwa na kufariki walichukua maaamuzi kuwafuata wafugaji walihohusika nao kuwapiga na kuwaua wafugaji wawili.
Wamesema kutokana na vurugu hizo, Kamati za Ulinzi na Usalama kutoka Nachingwea mkoani Lindi na Tunduru mkoani Ruvuma zikiongozana na wakuu wa wilaya hizo ziliwasili eneo la tukio kutaka kufahamu sababu ziliochangia kuzuka kwa vurugu hizo.
Wakiongea kwa nyajati tofauti katika eneo la tukio Wakuu hao wa Wilaya, Mohamedi Moyo (Nachingwea) na Julius Mtatilo (Tunduru) waliwataka wananchi kuendelee kuishi kwa amani na upendo bila ya kufanya vurugu kwani amani ni wajibu wa kila mwananchi.
“Tunachopenda kuwaeleza ni kuwa muendelee kuishi kwa amani, ikizingatiwa nyinyi mnaishi mpakani mwa Wilaya za Nachingwea na Tunduru” walisema kwa nyakati tofauti viongozi hao.
Akizungumzia kadhia hiyo Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, Pili Mande pamoja na mambo mengine amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa hata hivyo Diwani wa Kata ya Tinginya,Wilaya ya Tunduru Eliasa Mshamu (45) anashikiliwa kwa madai ya kuwashawishi wananchi kwenda kulipiza kisasi cha mauwaji kwa wafugaji hao pamoja na kuharibu mali kwa kuzichoma moto.
Kamanda Mande ametaja baadhi ya mali za wafugaji zilizoteketezwa kwa kuchoma moto ni pamoja na vibanda (15) vilivyotumika kuishi wafugaji.