Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Kibaha
Mbwa na Paka 4400 wanatarajiwa kuchanjwa dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha Mbwa kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha kuanzia Septemba 28,2023 ambapo hafla ya uzinduzi wa maadhimisho itafanyikia kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kongowe kuanzia Majira ya saa mbili asubuhi.
Aidha,zoezi la uchanjaji litazinduliwa rasmi na Mkuu Mkuu wa Divisheni ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Charles Marwa ambapo Mbwa na Paka 2200 idadi ambayo ni sawa na asilimia 50 ya wanyama tarajiwa kuchanjwa itafanyika siku ya awali
Deogratius Mgute ni Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Mji Kibaha amesema tayari dozi 700 zilizogharimu kiasi cha shilingi 1,190,000 kimepokelewa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi huku Ofisi ya Mkurugenzi Kibaha ikigharamia dozi 1500 kwa shilingi 2,550,000 na kufanya uwepo wa dozi 2200 zitakazo tumika kwenye kata 14 zenye jumla ya Mitaa 73.
Sambamba na chanjo Marwa amesema wataalam watatumia fursa hiyo kutoa elimu juu ya mbinu Bora za Ufugaji wa Mbwa na paka pamoja na kugawa vipeperushi kwa wafugaji ili waendelee kupata Maarifa zaidi kwani lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kutokomeza ugonjwa na vifo vitokanavyo na kichaa cha Mbwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amemshukuru Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuendelea kuwajali wananchi kwa kutuletea chanjo hizo kwani kwa hivi karibuni kumekuwa na vifo vitokanavyo na kichaa cha Mbwa.Hata hivyo ametoa rai kwa wananchi kuwatunza mbwa wao ili wasiendelee kuleta madhara na hofu mitaani.
Maadhimisho ya siku ya kichaa cha Mbwa Dunia hufanyika kila Septemba 28 ambapo Mwaka 2023 yamekuja na kaulimbiu isemayo ” Kichaa cha Mbwa Afya Moja,vifo sifuri”
Wito unatolewa na Wananchi kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa wataalam ili zoezi la uchanjaji lilete tija kwa maslahi mapana ya Taifa ,amesema Deogratius Mgute.