Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia mwanaume mmoja (jina limehifadhiwa) mkazi wa kijiji cha Kaloleni, Wilayani Songwe akituhumiwa kwa mauaji ya Editha Msokwa (38) na mtoto wake mchanga wa miezi sita, Esther Emanuel chanzo kikielezwa kuwa ni wivu wa mapenzi baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mkewe kumzaa mtoto nje ya ndoa.
Mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mwambani, Wilayani Songwe baada ya kujeruhiwa na wananchi,anadaiwa kumvizia mkewe akiwa amelala usiku na mtoto wake na kuwanyonga kabla ya kuuburuta mwili wa mkewe na kwenda kuuficha kwenye kibanda nje ya nyumba yao.
Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ,Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba 24, 2023.
Amesema mtuhumiwa alikamatwa baada ya kuokolewa na viongozi wa kijiji chini ya Mwenyekiti Laiton Waya kutoka katika kundi la wananchi wenye hasira kali waliomkamata mara baada ya kufanya tukio hilo la mauaji ya kinyama na kuanza kumshushia kipigo kikali.
“Mtuhumiwa huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mwambani akiwa chini ya ulinzi, na uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi unaonyesha kuwa mtuhumiwa kabla ya kutekeleza mauaji hayo walikuwa na mgogoro na mkewe kwa kumtuhumu kuwa kuzaa nje ya ndoa ” amefafanua Kaimu Kamanda Ngonyani.
Aidha, Kaimu Kamanda Nginyani amesema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na pindi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.