Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Viongozi na wataalam wa Mkoa wa Dar es Salaam leo Septemba 25, 2023 wameanza mafunzo ya siku mbili ya kujiweka sawa kukabiliana na athari zinazo weza kutokea endapo mvua kubwa za El-Nino zitanyesha siku za hivi karibuni kwa mujibu wa utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya hewa hapa nchini.
Akifungua mafunzo hayo jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge Jenista Muhagama amewataka washiriki wote katika kikao kazi hicho kujadiliana kwa kina namna ya kujipanga na kujiandaa kukabiliana na EL-NINO endapo itatokea, ni lazima kujiratibu na kuwa na vifaa na rasilimali zingine zinazoweza kutumika wakati wa kulikabili janga hilo.
Waziri ameutaka Mkoa huo kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma dhidi ya tukio hilo, kusafisha mito na kuimarisha kingo, kuainisha maeneo ambayo mara nyingi yana athari Kipindi cha mvua nyingi, kusimamia matumizi sahihi ya mitaro na mifereji ya maji taka pia kujipanga kuzuia athari na kutengeneza mipango ya kuzuia madhara pamoja na kushirikisha jamii katika ulinzi wa mito isiharibiwe.
Aidha kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hataki kuona wananchi wanapata athari za EL-NINO ndio maana ametoa maelekezo mahususi ya kujiandaa, kujipanga au kuweka mikakati ya kuzuia athari zinazoweka kutokea endapo mvua hizo zitanyesha.
Mkoa wa Dar es Salaam tayari umeshaanza kufanya maandalizi ya kukabiliana na EL-NINO ambapo tayari umeshaainisha maeneo hatarishi na kuanza kusafisha mito kwa mfano mto msimbazi vilevile kazi inaelea kusafisha mitaro na mifereji pia kuendelea kutoa elimu kwa Umma” amesema RC Chalamila.
Mwisho Waziri Mhagama baada ya kufungua mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na Kamati ya usalama ya Mkoa, Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, waratibu wa Maafa kutoka Wilaya zote, Sekretarieti ya Mkoa, wataalam kutoka TARURA, TANROAD na wadau wengine, amefanya ziara kujionea uhalisia katika maeneo ambayo yanaweza kuwa na athari kubwa ikiwemo Jangwani, mto Msimbazi, mto Ng’ombe, na mto mpigi unaotenganisha Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.