Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Manispaa ya Morogoro inaendelea na matengenezo ya barabara ili wananchi waweze kusafiri kwa urahisi.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Morogoro Mhandisi Mohamed Muanda alipokuwa akielezea utekelezaji wa miradi ya Wakala katika Manispaa hiyo.
Mhandisi Muanda amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha kwamba barabara zote za lami zilizojengwa muda mrefu zaidi ya miaka ishirini na kupelekea kuchakaa pamoja na kuwa na mashimo ya mara kwa mara (port holes) zinafanyiwa matengenezo makubwa na madogo.
“Kama mnavyofahamu Manispaa ya Morogoro ni njiapanda na barabara zake zinapitisha magari makubwa na madogo pande zote za nchi , sisi kama TARURA tumeona njia hii ni nzuri na itasaidia kuziongezea muda wa kuendelea kuishi ili kutoa huduma kwa muda mrefu” amesema.
Mhandisi Muanda ameongeza kuwa aina hiyo ya matengenezo ya barabara kwa kuongeza tabaka jingine la lami ( Overlay) kwa kuanzia wanaziba kwanza viraka vinavyotokea katika kila barabara na baadae wanachagua barabara moja ambayo inakua imezidiwa kutokana na kupitisha magari mengi na hivyo kuiongezea tabaka lingine la lami kwa juu.
Kwa upande wa kufungua barabara Mhandisi Muanda amesema kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa bajeti ya barabara imeongezwa kutoka Bil. 2.8 hadi kufikia Bil. 7.35 na kuwawezesha kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili wananchi.