*Imeagiza bei za vifaa vya ujenzi zishushwe nchini
*Tofauti ya kipato yaelezwa ikiachwa hivi italeta vurugu
*Ada shule binafsi zidhibitiwe, utozaji dola ukomeshwe
*Yakiri ajira ni bomu, wizara lazima ziandae ajira mpya
*Ushuru na vijikodi vinavyoumiza wananchi vikomeshwe
Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano wake Mkuu wa Nane uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, kilitoa maazimio ambayo kimeyaeleza kuwa ndiyo dira yake ya ushindi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Kutoka na umuhimu na maudhui yake kwa wanachama wake na Watanzania, na kwa kuzingatia kuwa CCM kama chama tawala kinapaswa kusimamia na kutekeleza ahadi zake, tumeona ni vema wasomaji wa JAMHURI wakapata na kuwa na kumbukumbu halisi ya Maazimio hayo, ili siku ya siku waweze kuhoji utekelezwaji wake.
MAAZIMIO YA MKUTANO WA NANE WA CCM TAIFA
TAREHE 11-13 NOVEMBA 2012
UTANGULIZI
Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefanyika chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 11 hadi 13 Novemba 2012. Mkutano huu wa Nane, una umuhimu mkubwa kwa kuwa unafanyika katika mazingira mahsusi; wakati:-
(i) Tanzania Bara ikiwa imeadhimisha miaka 50 tangu kupatikana Uhuru.
(ii) Chama Cha Mapinduzi kikiwa kimetimiza miaka 35 tangu kuzaliwa.
(iii) Tukiwa tunaelekea kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi adhimu ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
(iv) Taifa letu likiwa limeanza mchakato wa kuandika Katiba mpya itakayokidhi mazingira mapya na mahitaji ya Taifa lenye umri wa miaka 50.
(v) Chama chetu kikiwa kimeanza mchakato wa mageuzi ndani ya chama yenye nia ya kukiimarisha.
(vi) Miaka 25 ya mageuzi ya kiuchumi.
(vii) Mwaka mmoja baada ya kuundwa kwa SUKI Zanzibar.
Mkutano huu unaomalizika kwa mafanikio makubwa, umepokea, umetafakari na kujadili taarifa kuu tatu:-
Taarifa ya Halamashauri Kuu ya Taifa ya Kazi za Chama 2007-2012 kwa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa tarehe 11-13 Novemba 2012.
Taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi za:-
(a) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
(b) Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na taarifa hizi, wajumbe pia wamepata fursa ya kujadili mambo mengine makubwa na muhimu yanayohusu uimarishaji wa CCM na ustawi wa Watanzania na Taifa letu kwa ujumla.
Baada ya kujadili taarifa hizi pamoja na mambo mengine, Mkutano Mkuu umeona na kuazimia yafuatayo:-
1. Kuwapongeza wanachama wa CCM kwa kushiriki kwao kikamilifu katika kuandaa na kufanikisha Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM.
2. Kumpongeza Mwenyekiti wa Chama, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kusimamia maandalizi hayo na kuendesha kikao kwa ufanisi mkubwa. Aidha, tunampongeza kwa hotuba nzuri ya ufunguzi iliyozungumzia maeneo yote yanayohusu maendeleo ya wananchi na ustawi wa nchi yetu. Mkutano Mkuu unaiagiza Halmashauri Kuu ya Taifa kutengeneza programu ya utekelezaji wa maudhui yaliyomo kweye hotuba hiyo.
3. Kuzipongeza Serikali zote mbili – ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi 2010, ambao ndiyo mkataba kati ya Chama Cha Mapinduzi na Watanzania.
Muungano
Mkutano Mkuu unatambua na kuthamini umuhimu wa kuuenzi na kuuimarisha Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, kama njia ya kuthamini jitihada za wananchi wa pande zote mbili kujenga na kuimarisha udugu, umoja na mshikamano wao.
Chama Cha Mapinduzi kinatambua kuwapo na changamoto za Muungano na kuzitafutia majawabu kila inapobidi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Mkutano Mkuu unapongeza kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ambayo imeweza kuwaunganisha Wazanzibari na kupata mafanikio makubwa. Mkutano Mkuu unawahimiza Watanzania wote wenye nia njema kuendelea kuiunga mkono.
Umoja wa Kitaifa
Mkutano Mkuu unatambua kazi kubwa iliyofanywa na Chama chetu katika kujenga umoja, udugu, amani na mshikamano miongoni wa Watanzania. Mkutano Mkuu unawahimiza Watanzania kuendelea kuuthamini na kuuenzi umoja huo kama kielelezo cha Watanzania na msingi wa maendeleo ya nchi yetu. Mkutano Mkuu unatoa wito kwa Watanzania kutokubali harakati za baadhi ya watu kutugawa kwa misingi ya udini, ukabila, rangi, ubara na uzanzibari na tofauti nyingine zozote.
Ujenzi wa Uzalendo
Uzalendo na utaifa itaendelea kuwa misingi muhimu ya ujenzi wa Taifa letu. Mkutano Mkuu unahimiza kuchukuliwa hatua madhubuti za kufundisha na kukuza uzalendo hasa miongoni mwa vijana wetu kwa kupitia mitaala shuleni na katika taasisi mbalimbali.
Uimarishaji wa Chama.
CCM ni chama chenye historia adhimu na dhamana kubwa ya uongozi wa nchi. Mkutano Mkuu unaamini kwamba uimara wa CCM unatoa uhakika wa ustawi wa Taifa letu. Mkutano Mkuu umeona haja ya kuendelea na jitihada za kujenga na kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.
Mkutano Mkuu unawaagiza viongozi wa Chama katika ngazi zote kuongeza jitihada za kuwa karibu na wananchi, na kuwasemea na kuwatetea. Mikutano kati ya viongozi wa Chama na wananchi kufafanua na kuelezea mambo mbalimbali ifanyike mara kwa mara.
Mkutano Mkuu unaagiza kasi iongezwe kwenye utekelezaji wa mageuzi ndani ya Chama yenye malengo ya kukiimarisha.
Maadili, Nidhamu, Matumizi Mabaya ya Madaraka na Uwajibikaji
Mkutano Mkuu unatambua mwenendo wa kumomonyoka kwa maadili, nidhamu pamoja na uwajibikaji miongoni mwa baadhi ya viongozi na watendaji ndani ya Chama na serikalini.
Mkutano Mkuu unaiagiza Serikali pia unahimiza kuwachukulia hatua kali na za haraka, wale wanaotenda kinyume cha misingi ya maadili ya uongozi na utendaji kazi.
1.2 Mkutano Mkuu vile vile unahimiza utekelezaji wa mageuzi yahusuyo viongozi wa ngazi za juu kutembelea wanachama na wananchi matawini, vijijini na mitaani na kufanya mikutano ya hadhara ili kuelewa kero zao na kuzitafutia majawabu. Utaratibu wa umangimeza haufai na haukubaliki katika kuongoza Chama Cha Mapinduzi, kwa wakati huu wa siasa za ushindani. Aidha, utaratibu mpya wa kuwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika ngazi ya Wilaya, unalenga kuongeza nguvu katika ngazi ya Wilaya ya kutembelea na kuhudumia ngazi za chini na hasa katika kutatua kero za wananchi itumiwe kikamilifu.
4. Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
Mkutano Mkuu unaziagiza Serikali zote mbili zitekeleze kwa ufanisi sera ya kuwawezesha wananchi wote wanufaike na rasilimali za nchi yao, ili hatimaye waondokane na umasikini. Maeneo yafuatayo yapewe kipaumbele:-
4.1 Kuimarisha shughuli za Ushirika
Mkutano Mkuu unatoa wito kwa Halmashauri Kuu ya Taifa na Serikali za CCM kuhamasisha na kusimamia kwa nguvu zaidi Ushirika ambao ndiyo nguzo kuu ya utekelezaji wa Sera ya Ujamaa na Kujitegemea. Shughuli zote zenye mwelekeo wa kiushirika zipewe msukumo stahiki kwa mfano ushirika wa mazao, ufugaji, uvuvi, SACCOS, VICOBA.
4.2 Mikopo nafuu
Mkutano Mkuu unaihimiza Serikali kutekeleza Sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, kama ilivyofafanuliwa kwenye Waraka wa Mwelekeo wa Sera za Kiuchumi za Miaka ya 1990-2000, kwa kuhakikisha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya mitaji kwa urahisi na kwa masharti nafuu na iwafikie wananchi wote wa mijini na vijijini.
4.3 Kusaidia Wafanyabiashara Wadogo Wadogo
Mkutano Mkuu unaziagiza Serikali kutekeleza yafuatayo:-
(a) Halmashauri zitenge maeneo mahsusi kwa ajili ya biashara ndogo ndogo.
(b) Halmashauri ziondoe kero na malalamiko kuhusu kodi na ushuru zinazokwamisha jitihada za wafanyabiashara wadogo wadogo za kujikwamua kimaisha.
(c) Halmashauri ziwe na mipango ya kuwezesha kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo hasa waliojiunga katika vikundi.
4.4 Wananchi Kumilikishwa Ardhi
Mkutano Mkuu unatambua umuhimu wa rasilimali ardhi kama nyenzo ya kusaidia mapambano dhidi ya umasikini. Kwa hiyo inaagiza kama ifuatavyo:-
a. Serikali iharakishe kazi ya kupanga matumizi bora ya ardhi, kuipima, na kuwamilikisha wananchi mijini na vijijini.
b. Migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, na pia baina ya wananchi na wawekezaji inayojitokeza katika baadhi ya mikoa, ipatiwe ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.
4.5 Kuhusu Tatizo la kukua kwa pengo la mapato katika jamii
Mkutano Mkuu unasikitishwa na hali inayojengeka ya kukua kwa kasi pengo la mapato baina ya walio nacho na wasio nacho, na kwamba Serikali zote mbili zinaagizwa kuchukua hatua za kurekebisha hali hii mapema, kwani ikiachwa iendelee itajenga chuki, na uhasama baina ya matabaka haya mawili, na hivyo kuathiri amani na umoja wa Taifa letu.
5. Kuhusu Tatizo la ajira Nchini
Mkutano Mkuu baada ya kupokea taarifa ya Serikali kuhusu hatua zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo la ajira, hasa kwa vijana, umetoa maelekezo yafuatayo:-
i. Kila mwaka Wizara iwekewe lengo la kuzalisha ajira mpya na mwisho wa mwaka tathmini ifanywe iwapo malengo yamefikiwa na kila Wizara.
ii. Shughuli za sekta isiyo rasmi, na hasa biashara ndogo ndogo, wachimbaji wadogo wadogo, mama lishe, wavuvi, wakulima wadogo, wafugaji nyuki, n.k ziwekewe mikakati ya kusaidiwa kimtaji, mafunzo na zana ili sekta hii iweze kuajiri watu wengi zaidi kuliko ilivyo sasa.
iii. Serikali iangalie uwezekano wa kutoa msamaha wa kodi na ushuru kwa wajasiriamali wanaoanza uzalishaji, ili kuwawezesha kukuza shughuli zao, na hatimaye wajiajiri wenyewe na hivyo kupunguza idadi ya watu wasio na ajira nchini.
6. Kuboresha masilahi ya Wakulima na Wafanyakazi
Kwa kutambua ukweli wa kihistoria kwamba CCM ni Chama cha kupigania haki za Wakulima na Wafanyakazi, na kwa kuelewa kwamba CCM ndicho Chama pekee ambacho kina historia ya kutetea masilahi ya makundi haya; Mkutano Mkuu unaziagiza Serikali zote mbili kuchukua hatua zifuatazo kwa lengo la kuboresha masilahi ya Wakulima na Wafanyakazi:-
(a) Wafanyakazi
i. Kuhakikisha kila inapowezekana Serikali inaongeza kipato cha wafanyakazi ili kiende sambamba na upandaji wa gharama za maisha. Sekta binafsi pia isimamiwe itekeleze azma hii ya CCM.
ii. Uboreshaji wa mapato ya wafanyakazi uendane na kuboresha mazingira ya kazi; hasa kuwapatia wafanyakazi vitendea kazi vya kisasa na vya kutosha, pia kupatikana kwa huduma za nyumba vijijini kwa walimu, waganga na maafisa ugani mbali mbali.
iii. Wafanyakazi walio katika maeneo yenye mazingira magumu wawekewe utaratibu wa kupunguza ukali wa maisha.
(b) Wakulima
i. Serikali isaidie kutatua tatizo la nishati vijijini kwa kushusha bei ya mafuta ya taa, yanayotumiwa na wananchi walio wengi vijijini; pia kuongeza kasi ya usambazaji nishati ya umeme.
ii. Serikali ziboreshe utaratibu wa kusambaza pembejeo zenye ruzuku ili ziwafikie wakulima wengi zaidi na kwa muda mwafaka.
iii. Kupitia utekelezaji wa mpango wa Kilimo Kwanza, Serikali iweke utaratibu wa kuimarisha masoko ya ndani na nje ya nchi kwa mazao ya wakulima, na hasa pamba, kahawa, korosho na mahindi ili wapate bei zenye masilahi kwao, na pia iweke utaratibu bora na wenye bei nafuu wa upatikanaji zana za kisasa za kilimo, pia dawa za mimea na za mifugo.
7. Kuhusu usambazaji wa Huduma za Jamii kwa wote
Mkutano Mkuu unatambua kwamba usambazaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wote, ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea, hivyo Serikali zote mbili zinahimizwa kutekeleza yafuatayo:-
7.1 ELimu
Serikali ya Muungano inaagizwa kutazama uwezekano wa kuanza mchakato wa kuifanya elimu ya sekondari nchini kuwa ya wote, ili fursa ya elimu ya sekondari ipatikane kwa watoto wote na iwe ni haki ya msingi kwa kila mtoto hapa nchini.
Vile vile jitihada za hivi sasa za kuboresha elimu ya msingi na ya sekondari kwa kuondoa tatizo la upungufu wa walimu, na kuongeza vitendea kazi hasa madawati, madarasa, maabara na nyumba za walimu ziendelezwe kwa kasi zaidi.
Hali kadhalika, Serikali isimamie kwa ukamilifu kudhibiti viwango vya ada binafsi ikiwamo suala la kulipa ada kwa dola.
7.2 Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
Kuhusu upatikanaji wa elimu ya chuo kikuu, Serikali iweke utaratibu utakaowawezesha wanafunzi wote wenye sifa ya kujiunga na vyuo vikuu wapate mikopo. Utaratibu wa sasa ambao mikopo inategemea fedha za bajeti ya Serikali utazamwe upya kwa kuwa hauwezeshi wanafunzi wote wanaohitaji mikopo kuipata.
7.3 Huduma za Afya
Kuhusu utoaji wa huduma za afya, Mkutano Mkuu unaiagiza Serikali kuimarisha utaratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) mijini na vijijini ili utumike kutoa huduma bora za afya na zilizo nafuu kwa wananchi wote na hasa kuondoa tatizo la upungufu wa dawa katika zahanati na vituo vya afya na pia upungufu wa vifaa tiba.
7.4 Huduma ya Maji
Mkutano Mkuu unazitanabaisha Serikali zote mbili kwamba hivi sasa maji ni mojawapo ya huduma zenye changamoto kubwa hapa nchini. Vilio vya uhaba wa maji safi na salama vinasikika mahali pengi nchini; mijini na vijijini. Hivyo, Mkutano Mkuu unaziagiza Serikali zote mbili ziweke mipango mahsusi ya kugharimia usambazaji wa miradi ya maji, mbali ya mpango wa sasa unaotegemea mkopo wa Benki ya Dunia. Kero ya maji ina uzito wa pekee na hivyo Serikali ziweke mipango mahsusi ya kuitafutia ufumbuzi kati ya sasa hadi 2015.
7.5 Usambazaji wa Huduma ya Umeme
Mkutano Mkuu unatambua umuhimu wa umeme kama kichocheo cha maendeleo ya kisasa mijini na vijijini; kwa kutambua hali hiyo unatoa maagizo yafuatayo:-
a. Serikali itekeleze kwa makini mpango kabambe wa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini (National Power Master Plan) hasa kupitia vyanzo vipya vya umeme unaotokana na gesi, makaa ya mawe, upepo na jua (solar).
b. Usambazaji umeme vijijini kupitia Wakala wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA), upewe msukumo mkubwa zaidi kwani hadi sasa huduma ya usambazaji umeme vijijini ipo chini sana (17%).
8. Ujenzi wa Nyumba Bora na za Bei Nafuu
Mkutano Mkuu unaziagiza Serikali zote mbili zitoe kipaumbele katika suala la ujenzi wa nyumba, kwani upatikanaji wa nyumba bora kwa Watanzania ni jambo muhimu katika mapambano dhidi ya maisha duni.
Mkutano Mkuu unaiagiza Serikali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kuhusu sekta hii ichukue hatua zifuatazo:-
a. Kutoa motisha kwa ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu kwa kuondoa kodi katika vifaa vya ujenzi wa nyumba kama vile saruji, mabati, nondo n.k.
b. Kuondoa kodi ya VAT katika nyumba za bei nafuu (low-cost housing) zinazojengwa na kuuzwa na mashirika ya kiserikali na ya sekta binafsi, ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu kuzinunua kwa njia ya mikopo.
c. Utaratibu wa mikopo ya kujenga au kununua nyumba urahisishwe kwa Benki Kuu kudhibiti riba. Mikopo ya aina hii kwa kawaida huwa ni ya muda mrefu (miaka 10-25), hivyo riba ikiwa kubwa, mikopo inakuwa ni mzigo usiobebeka kwa wananchi wenye kipato cha chini.
d. Serikali ianzishe taasisi itakayosimamia na kudhibiti kodi za pango la nyumba ambazo hivi sasa ni kubwa mno na zinatozwa kwa mwaka mzima, hivyo kuwatesa wapangaji, hususani wa kipato cha chini.
10. Mapambano dhidi ya Rushwa
Mkutano Mkuu unalaani tabia ya baadhi ya wagombea uongozi kutoa rushwa nyakati za uchaguzi na unaiagiza Halmashauri Kuu ya Taifa kuchukua hatua kali dhidi ya watakaothibitika kujihusisha na tabia hii ikiwa ni pamoja na kutengua matokeo ya ushindi wao.
11. Kuimarisha Maadili na Miiko ya Uongozi
Mkutano Mkuu unasikitishwa na wimbi lililozuka la baadhi ya viongozi kutumia nafasi zao kujitajirisha, hali inayosababisha madhara makubwa kimaadili na kiuongozi. Mkutano Mkuu unaiagiza Serikali kuchukua hatua za kuondoa mgongano huo wa kimasilahi (conflict of interest) kwa kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Miiko ya Uongozi, na pia iharakishe hatua za kuweka sheria itakayotenganisha mtu kuwa kiongozi wa umma na mfanyabiashara kwa wakati mmoja. Lengo ni kurejesha dhamira ya Azimio la Arusha la kuwa na viongozi wanaotumikia umma kwa masilahi ya umma, na siyo viongozi wanaotumia ofisi za umma kwa masilahi binafsi.
12. Kudhibiti Makundi ndani ya Chama
Mkutano Mkuu unakemea tabia iliyojitokeza miaka ya hivi karibuni, ya uundaji wa makundi ya kiuhasama ndani ya Chama. Makundi haya huanzia nyakati za uchaguzi, lakini uchaguzi unapoisha, yenyewe hubaki ili kujiandaa kwa uchaguzi unaofuata. Matokeo ya uwepo wa makundi haya ni hatari kwa uhai wa Chama chetu, kwani yanakigawa Chama, yanachochea fitina na chuki miongoni mwa wanachama, na kwa jumla yanadhoofisha nguvu za Chama chetu. Kwa hali hii Mkutano Mkuu unaiagiza Halmashauri Kuu ya Taifa iwashughulikie vinara wa makundi haya kwa lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa Chama chetu.
13. Pongezi
Kadhalika, Mkutano Mkuu unaipongeza Halmashauri Kuu ya Taifa iliyomaliza muda wake kwa kuongoza kwa ufanisi kampeni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2009 na Uchaguzi Mkuu wa 2010 na kukipatia Chama chetu ushindi mkubwa katika nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi, udiwani na Serikali za Vijiji/Mitaa na Vitongoji. Aidha, Halmashauri Kuu ya Taifa inapongezwa kwa kuanzisha mradi wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa mikutano na Ofisi za Makao Makuu ya Chama uliowekwa jiwe la msingi wakati wa Mkutano huu wa Nane.
14. Mwisho
Maazimio haya ya Mkutano Mkuu ndiyo maelekezo ya kazi kwa ngazi zote za Chama na Serikali zake, katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Maazimio haya yana lengo la kusukuma na kuhimiza utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kuimarisha Chama na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi (2010-2015), hasa kwa maeneo yenye uwezo wa kuinua hali ya maisha ya wananchi wa kawaida.
Aidha, Mkutano Mkuu unaiagiza Halmashauri Kuu ya Taifa iweke Mpango Kazi wa kuyatekeleza maazimio haya (Plan of Action), na kwamba kila mwaka Chama kifanye tathmini ya utekelezaji wake.
Mkutano Mkuu unasisitiza na kuagiza kwamba Chama katika ngazi zake zote kisimamie kwa ukamilifu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Mradi wa Awamu ya Tatu ya Kuimarisha Chama na pia utekelezaji wa mageuzi ndani ya Chama ili kuimarisha uhai wa Chama, na kudumisha umoja na mshikamano ndani ya Chama, ambazo ndizo silaha zetu muhimu za kuleta ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015.