Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amewataka wananchi kuyalinda na kuyaendeleza maeneo ya wazi kulingana na matumizi yaliyopangwa.
Silaa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kukagua maeneo ya wazi Mbweni jijini Dar es Salaam.
“Niwatake watanzania wengine wote wanaokaa katika maeneo ya wazi wayaprotect, yako maeneo Mwananyamala yamegeuzwa gerage, yapo mengine yamegeuzwa sehemu ya kutupa takataka hatuwezi kuwa na miji ya namna hiyo” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa, ni lazima mamlaka za kusimamia mipango miji na ardhi pamoja wananchi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao katika kuyalinda na kuyaendeleza maeneo ya wazi.
Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo na Makazi amesema, anayo orodha ndefu ya maeneo ya wazi yaliyofunguliwa biashara na asingependa maeneo hayo yakitumika kibiashara.
Ametaka watanzania wote kwa ujumla kuwa walinzi namba moja wa maeneo ya wazi ambapo alifafanua kuwa, zipo ‘open space’ nyingi leo hazipo na watu huanza kidogo kidogo kujenga ama biashara kwenye maeneo hayo.
Amezitaka halmashauri zote nchini kuendelea kuhamamisha wananchi kuyalinda na kuyaendeleza maeneo ya wazi kulingana na mipango iliyopo.
Ziara ya Waziri Silaa kukagua maeneo ya wazi Mbweni Dar es Salaam ni moja ya jitihada zake za kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa wakati akianza kuhudumu Wizara ya Ardhi ya kutaka maeneo yote ya wazi kubaki wazi ndani ya siku mia moja.