Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Serikali imesema itaendelea kupokea maoni ya wadau ya kuboresha sera za Uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana, wanawake na watu wenye Ulemavu katika sekta zote nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu Walemavu Protabas Katambi akizungumza katika Siku ya VICOBA Tanzania iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 23, 2023.
Katambi amesema katika kuboresha Uchumi wa Mtanzania, Serikali imefanya masuala mbalimbali ikiwemo kuwa na Mpango Maalum wa kuwa na mifuko ya kukopesha wananchi ili kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha biashara na shughuli za kiuchumi.
Ameitaja mifuko hiyo iliyopo kwenye Wizara za kisekta ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Pembejeo za kilimo na mifuko mingine iliyoanzishwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara yake ina jukumu la kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) unaotoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake. Mikopo hiyo imekuwa ikitolewa kwa riba ya 4% tu ili wanawake waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuondoa utegemezi kwa wanaume.
Ameongeza kuwa Wizara inatekeleza Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo kwa lengo la kuimarisha shughuli za maendeleo ya jamii, masuala ya wanawake na jinsia, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, huduma za wazee pamoja na masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto kwa lengo la kuwa na jamii yenye maendeleo endelevu.
“Ninawasihi sana wananchi hususan wanawake kutumia fursa hiyo kikamilifu ili waweze kujiinua kiuchumi na kuyafikia malengo yao kwani azma ya serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha kila mwananchi anaweza kukidhi mahitaji yake ya msingi kwa urahisi na kwa wakati.” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Kwa upande wake Rais YEMCO VICOBA Tanzania Mohamed Basanga ameiomba Serikali kuweka uratibu katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri hasa kwa kuziangalia Taasisi ya Vicoba kuwezesha ziweze kuwalea wajasirimali wadogo wadogo katika kupata mikopo yenye riba nafuu ili kukuza bidhaa biashara zao.
“Mhe. mgeni rasmi nikuombe ufikishe salamu zetu kwa Rais Samia atukumbuke Taasisi za Vicoba katika fedha za Uwezeshaji ili ruweze kuwainua wajasirimali wengi na kujenga Uchumi wa Nchi” amesema Basanga