Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD), imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 500 kwa hospitali ya Wilaya ya Ilala (Kivule), lengo ni kuboresha hali ya utoaji huduma wilayani humo.
Vifaa hivyo ni pamoja na Vitanda vya kulalia wagonjwa, ventileta za ICU, viti mwendo, friji za kuhifadhia damu na sampuli, vitanda vya uchunguzi, Sunction machine, Ultra Sound machine, magodoro na mashuka.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Dk. Zaituni Hamza, ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa ujio wa vifaa hivyo, kwani vinaakisi adhma na dhamira ya kuboresha huduma za afya nchini.
” Tunamshukuru sana Rais wetu, hakika anafanya kazi kubwa sana katika sekta ya afya, ameboresha miundombinu ya utoaji huduma mathalani ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba, ajira na upatikanaji wa dawa, hii ni dhahiri kwamba anajali wananchi wake,”alisema.
Aliongeza kuwa, huduma za mama na mtoto kwasasa zimeboreka kuliko wakati mwingine wowote, hali ambayo inasababisha kupungua kwa vifo vya wajawazito na watoto wachang wakati wa kujifungua.
Katika hatua nyingine, alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, kwa maboresho ya huduma, ambapo kwa sasa zimeimarika, mawasiliano yameboreshwa kati ya bohari na wateja wake hali inayosababisha hospitali kupata msaada wa haraka pale wanapokua na uhitaji.
Alisema hatua hiyo imesababisha ongezeko la upatikanaji wa bidhaa za afya.
Alisema, hali ya upatikanaji wa dawa ndani ya jiji la Dar es Salaam ni zaidi ya asilimia 92 kwa dawa muhimu na hivyo hakuna mwananchii anayekwenda kituoni na kukosa dawa muhimu.