Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia amefungua kiwanda cha vifaa vya ujenzi (Sapphire Float Glass Tanzania), chenye thamani ya dola za Marekani milioni 311.
Akizungumza wakati anafungua kiwanda hicho leo Mkuranga, mkoani Pwani amesema kuwa tukio hilo ni muhimu kwa sekta ya viwanda na uwekezaji nchini, na kuwa uanzishwaji wa viwanda umeendelea kuongezeka.
“Pwani ina idadi ya viwanda 1525 , Kituo cha Uwekezaji (TIC) hadi kufikia Septemba mwaka huu imesajili viwanda 417 vyenye thamani ya shilingi trilioni 12”, amesema Rais Samia.
Kuhusu bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho, Rais Samia amesema kuwa asimilia 75 ya bidhaa zitauzwa nje ya nchi na asilimia 25 nchini.
Aidha, Mhe Rais Samia amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na tayari imefanya maboresho mengi ya kisera na kanuni ili uwekezaji kuwa na mazingira bora. Pia, mwaka 2022 imerekebisha kanuni ili kufanya uwekezaji kuwa na tija zaidi.
Ameongeza “Serikali inaendelea kuwekeza kwenye mifumo ya utoaji huduma, ili kurahisisha usajili na kutoa kutoa huduma kwa wawekezaji. Napenda kutumia fursa hii kuyahakikishia makampuni yote yaliyowekeza nchini kuwa mali zao ziko salama”.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa mradi huo unatarajia kuingiza nchini fedha za kigeni milioni 180 kwa mwaka.
“Hapa zimepatikana ajira sasa 750, kiwanda hiki kikikamilika zitapatikana ajira 1650. Vilevile, tunao uwezo wa kuhakikisha asimilia 100 ya malighafi zinazohitajika zinapatikana Tanzania”, ameeleza Waziri Kijaji.
Amefafanua kuwa kiwanda hicho kinatumia madini ya soda ash na chuma ambayo yanachukuliwa nje ya nchi, licha ya kuwa madini hayo yanapatikana nchini.
“Tumeanza mazungumzo na kiwanda hiki ili asilimia 100 ya malighafi zinazohitajika zipatikane ndani ya nchi”, amebainisha Waziri Kijaji.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wangkang Investment Group, Bw. Frank Yang amesema kuwa kiwanda hicho ni cha nne kwa ukubwa katika Bara la Afrika na wateja wa bidhaa zao wanatoka ndani ya nchi za Jumuiya Afrika Mashariki na SADC.
” Umuhimu wa mradi huu ni kuhakikisha Tanzania inaongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotengenezwa kwa kioo pamoja na kukuza ushirikiano wa Tanzania na China
Aidha, Mhe. Rais Samia amehitimisha ziara yake kwa kufungua kiwanda cha vifaa vya ujenzi katika Mkoa wa Pwani.