Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma
Wakazi wa Halmashauri ya Songea Vijijini wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji wa makaa ya mawe ambayo inatarajia kuleta tija kwa watanzania kutokana na uhitaji mkubwa wa madini hayo ndani na nje ya Nchi.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Matimila B na Liula, Wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayovutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali Duniani kuja kuwekeza na kufanya biashara ya madini yakiwemo makaa hayo.
Jenista amesema uwepo wa madini hayo utafungua milango ya kiuchumi ikiwemo ajira za muda mfupi na za kudumu akisisitiza ushirikishwaji wa wazawa hasa vijana katika uwekezaji huo kwa kuzingatia taaluma na uwezo wao kama sehemu ya kutambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa na kujikwamu kiuchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Hawa wawekezaji watakapoanza kazi zao wazingatie ushirikishwaji wa wazawa hasa vijana wetu wa hapa Matimila ajira zitakazozingatia taratibu na sheria za kazi badala ya kuendelea kusubiri ajira za serikalini tuanze kwa kuwatumia katika miradi yetu na uwekezaji ili wanufaike na kuleta mabadiliko katika maeneo yetu,” amesema Jenista.
Pia ameleza kuwa wanatarajia kuanzisha kiwanda cha shamba la kilimo cha miwa katika maeneo ya Muhukuru ndani ya Wilaya ya Songea kitakachozalisha sukari itakayotumika katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Nchi hatua itakayolitangaza Jimbo la Peramiho kwa kuweka historia ya mageuzi ya kiuchumi dhamira ya uwekezaji inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha ametoa wito kwa wakazi hao kuwekeza nguvu zao katika kilimo hasa kilimo cha mahindi akisema hivi sasa limekuwa zao la biashara badala ya kutumiwa kama chakula pekee kwani lina uwezo wa kubadilisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, kuwezesha kuhudumia familia, kusomesha watoto na huduma zingine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matimila Menas Komba ameahidi kutoa kiasi cha shilingi Milioni 40 kupitia mapato ya Halmashauri hiyo ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kiheo huku Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Jenista Mhagama akiahidi kutoa mifuko 150 ya saruji.
“Sisi kama Halimashauri kupitia mapato ya ndani tutatoa kiasi cha shilingi Milioni 40 ili kununua vifaa vya umaliziaji (finishing) kwani mpaka sasa imefikia asilimia 90 lengo kubwa ni wananchi wapate huduma ya afya katika maneo yao badala ya kutembea umbali mrefu kwenda mjini kutibiwa,”Ameeleza Mwenyekiti huyo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Zahanati ya Matimila B Afisa Mtendaji Kijiji cha Matimila B Omary Kamale ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kuhakikisha Zanahati na vituo vya afya vinajengwa na wananchi wanapata huduma muhimu ya afya.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Uoteshaji Uyoga Kijiji cha Matimila B Bi. Kotide Komba amemuomba Mbunge huyo kuwasadia kutatua changamoto zinazwakabili zikiwemo mitaji, masoko pamoja na vifaa vya kuongeza thamani ya zao hilo katika kikundi hicho cha uoteshaji uyoga kilimo ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwao kiuchumi kama wazee.