Na WMJJWM, Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirika la SOS Children’s Villages wamekubaliana kuendelea kuwekeza katika mikakati ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili kuondokana na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameyasema hayo wakati akizungumza na rais wa Shirika la SOS Children’s Villages Dkt. Dereje Wordofa katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar-es-Salaam.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wadau wote wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha Mashirika yanatoa huduma bora na stahiki kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo nchini kwa maslahi ya wananchi.
Aidha, amepongeza jitihada zinazofanywa na SOS Children’s Villages za kutoa huduma kwa wananchi wa Tanzania kwa kuzingatia sheria na mikataba ya Kimataifa ambayo nchi imeiridhia na kuongeza wigo wa huduma kutoka zile za kuhudumia watoto kwenye Makao hadi kushiriki kwa kutoa mchango wa kitaalamu na fedha kwenye uandaaji wa Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali ya huduma za Ustawi wa Jamii nchini.
“Matarajio ya Serikali ni kuona Shirika hili linaendelea kutoa mchango wa kitaalamu na rasilimali fedha katika kuimarisha huduma za kijamii kwa wananchi kupitia miradi inayoitekeleza na kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara.” Amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Amevitaja vipaumbele vya Wizara ni pamoja na kukamilisha mchakato wa uandaaji wa rasimu ya Sheria ya Huduma za Ustawi wa Jamii nchini, kukamilisha mapitio ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13 na Kanani zake na kukamilisha Rasimu ya Muundo wa Idara ya Ustawi wa Jamii.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha masuala ya ulinzi wa mtoto hususan uimarishwaji wa Mifumo ya Malezi Mbadala na afua za Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mitaani, Kuandaa Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Ustawi wa Jamii nchini, Kuimarisha afua za kuzuia na kupambana na ukatili wa Kijinsia na Ukatili Dhidi ya Watoto na Kuandaa Mwongozo wa Majukumu ya Wataalam wa Ustawi wa Jamii kwa kila Sekta.
“Shirika hili limekuwa mdau mkubwa wa Serikali katika utekelezaji wa miongozo ya uimarishaji wa mifumo na utoaji wa huduma kwa watoto na familia zilizo katika mazingira hatarishi hususan watoto na familia zilizo katika mkoa wa Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Zanzibar na maeneo mengine ya nchi” alisisitiza Naibu Waziri Mwanaidi
Kwa upande wake rais wa Shirika la SOS Children’s Villages Dkt. Dereje Wordofa amesema Watoto wengi wanakosa huduma muhimu kutokana na wazazi au walezi kutowekeza kwa watoto wao hasa katika kipindi cha malezi na Makuzi hivyo ni muhimu kuwekeza kwao ili kuwa na jamii iliyo imara.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii Nchini Dkt. Nandera Mhando amesema Shirika hilo limekuwa na msaada Mkubwa kwa jamii ya Kitanzania kwani limeanzisha vijiji ambavyo vinalea na kutunza Watoto wasio na wazazi au walezi na wale waliopo katika mazingira hatarishi na kutimiza ndoto zao za kupata huduma mbalimbali muhimu ikiwemo elimu na Afya.