Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbarali, Bw. Missana Kwangura amemtangaza Bi. Bahati Ndingo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi wa kiti cha Ubunge wa Jimbo hilo baada ya kupata kura 44,334 kati ya kura 56,095 halali zilizopigwa kwenye vituo 490 vya kupigia kura.
Bi. Ndingo amewashinda wagombea wengine 12 ambao walikuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika jana tarehe 19 Septemba, 2023.
Kwenye uchaguzi huo ushindani mkubwa ulioneka ukiwa baina ya Bi. Ndingo na Bw. Modestus Kilufi aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, aliyepata kura 10,014.
Akitangaza matokeo hayo Wilayani Mbarali leo tarehe 20 Septemba, 2023 Bw. Kwangura amesema wapiga kura yalioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Jimbo la Mbarali ni 185,836 ambapo kati yao 56,662 ndio waliopiga kura. Ameongeza kuwa kura halali ni 56,095 na kura zilizokataliwa ni 567.
Wengine waliokuwa wanagombea Ubunge kwenye Jimbo hilo na idadi ya kura walizopata ni Halima Abdalah Magambo (AAFP) aliyepata kura 336, Osward Joseph Mndeva (DP) aliyepata kura 130, Zavely Raurent Seleleka (UDP) aliyepata kura 158, Exavery Town Mwataga (CCK) aliyepata kura 118 na Morris Thomas Nkongolo (TLP) aliyepata kura 139.
Wengine ni Mary Moses Daudi (UPDP) aliyepata kura 113, Fatuma Rashidi Ligania (NLD) aliyepata kura 105, Bariki Oswald Mwanyalu (Demokrasia Makini) aliyepata kura 207, Hashim Abasi Mdemu (ADC) aliyepata kura 173, Mwajuma Noty Mirambo (UMD) aliyepata kura 113 na Husseni Hasani Lusewa kutoka Chama cha ADA- TADEA aliyepeata kura 155.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Mbarali umefanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Francis Mtega kilichotokea tarehe 01 Julai, 2023 kwa ajali ya kugongwa na trekta dogo (power tiller).
Sanjari na uchaguzi huo wa Ubunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya uchaguzi mdogo kwenye kata sita za Tanzania Bara ambapo matokeo yaliyotangazwa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa kata zilizofanya uchaguzi yanaonesha kuwa Bw. Helman Masila wa CCM ameshinda kwenye Kata ya Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Bw. Kayombo Christopher Fabian ameshinda kwenye Kata ya Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Matokeo mengine yanaonesha kuwa Bw. Ng’wanza Venance Mathias ameshinda kwenye Kata ya Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw. Peter Dastan Massawe wa CCM ameshinda katika Kata ya Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Bw. Simon Rogath Massawe wa CCM ameshinda katika Kata ya Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Bw. Diwani Twaibu Ngonyani wa CCM ameshinda katika Kata ya Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.