Mzee Ali Hassan Mwinyi alipata kusema maneno haya: “ Tanzania ni sawa na kichwa cha mwendawazimu.” Maneno haya aliyasema kwa maana kwamba kichwa cha mwendawazimu kila anayejifunza kunyoa hufanyia hapo mazoezi. Wiki iliyopita nilikuwa Nairobi , Kenya ambako nilikuwa na mafunzo ya wiki zaidi ya mbili. Nikiwa huko kwa mshangao nikakuta Tanzania inamwagiwa sifa.
Wakenya wanaimwagia sifa Tanzania kuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji kodi. Wanasema Mamlaka ya Mapato Tanzania imefanikisha kuweka mashine za elektroniki zinazotumika kutoa risiti kwa kila mteja anayenunua bidhaa yoyote. Kauli hii ilinitia mshituko wa mwaka. Nikajua Kenya wanaangalia takwimu, na si mwenendo.
Kwanza kabla sijazungumzia hizo risiti za elektroniki (ETR) ni vyema nikazungumzia mfumo mzima wa uchumi katika nchi hii. Nchi hii wafanyabiashara sasa wanafanya watakalo. Wanauza bidhaa bila kutoa risiti na ukidai risiti wanakwambia unaongezewa bei. Hii maana yake nini? Ni onyo kwa wale wenye kudai risiti kuwa watauziwa kwa bei ghali. Baada ya onyo hili inakuwaje? Wanunuzi wote hawadai risiti.
Wanunuzi wasipodai risiti inakuwaje? Mwenye duka au baa haijulikani anauza kiasi gani, hivyo kamwe au milele halipi kodi. Ndiyo maana unakuta maduka makubwa yenye kuuza mabilioni hadi leo yanajiendesha kwa kutumia leseni ya business name, ambayo gharama yake ni Sh 6,000 tu. Ndiyo maana wenye baa ukiomba tunachokiita bili anakuletea kiji-karatasi kilichochanwa kutoka kwenye daftari la shule, akiwa na uhakika kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawawezi kupata kumbukumbu hizo.
Hali inakuwa mbaya zaidi. Wenye maduka na machinga wanapandisha bei watakavyo. Ndiyo maana unakuta juisi ya Azam kuna mahala inauzwa kati ya Sh 2,000 na 3,500. Ndiyo maana unakwenda kwenye maduka kama ya Star Times ukiwa umepoteza smart card ukienda Buguruni unaambiwa smart card inauzwa Sh 25,000 lakini ukienda makao makuu Mikocheni inauzwa Sh 10,000.
Hapa kwetu chini ya uongozi wa awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa, tulianzisha kitu kinachoitwa soko huria. Kwa bahati mbaya Mkapa alidhani kuwa Watanzania wameendelea sawa na Wazungu. Kwamba kwa Wazungu kumwibia mtu kwa kupandisha bei wanajua fika kuwa ni kuua biashara, lakini hapa kwetu ni ujanja.
Sitanii, unakuta eneo kama Mnazi Mmoja mfanyabiashara anamiliki maduka matatu ya vitenge. Kitenge kile kile, lakini duka moja anakiuza Sh 20,000 huku kwingine akikiuza Sh 12,000. Ukiuliza unapewa majibu rahisi. Eti ni biashara huria, kumbe ni biashara holela. Ulaya kuna maadili. Mteja akigundua kuwa mwenye duka kamwibia kwa kumlangua, anaruhusiwa kwenda kulalamika kwenye Baraza la Walaji au Tume ya Ushindani wa Haki.
Vyombo hivyo hapa kwetu vipo, lakini utavisikia pale tu Pepsi wanapogombana na CocaCola au Serengeti Breweries na TBL. Vinginevyo ni kama vipo likizo. Baraza la Walaji ndo usiseme kabisa. Inawezekana hata wewe msomaji umelisikia hapa nilipolitaja, lakini hukujua kuwa kuna chombo kama hicho chenye jukumu la kutetea wananchi dhidi ya wafanyabiashara wenye kuwalangua wateja.
Nchi kila pahala ni vurugu. Kwenye eneo la ada za shule ndo usiseme. Kila mwenye shule akiamka asubuhi anaongeza ada. Katika mazingira ya kawaida hutarajii ada ya shule iongezeke kutoka Sh 800,000 hadi Sh 1,700,000 bila maelezo ya msingi huku wenye shule wakiwaambia wazazi kama msipotaka kuleta watoto wenu hapa shuleni, acheni.
Sitanii, ugonjwa huu umekwenda hadi kwenye vyuo vikuu binafsi. Mwaka jana vilipoambiwa kupunguza ada vikatunisha msuli. Kipo chuo kimoja ambacho kinafundisha sheria taarifa nilizopata kimeanza kupata adhabu. Mwaka jana kilipata wanafunzi 300, lakini mwaka huu kutokana na kupandisha ada kwa kiwango cha kuwanyima watoto fursa, kimepata wanafunzi 45 tu.
Chuo hiki kimejitanua nchi nzima, kinajenga majengo marefu kama hawana akili nzuri, lakini kumbe wamesahau kuwa kuna kiwango cha kumkamua ng’ombe. Ukiendelea kumkamua ng’ombe aliyekausha maziwa, utaishia kukata chuchu. Hata machinga wameiga mchezo huu, sabuni zilizokuwa zinauzwa nne kwa Sh 1,000 sasa hivi wanasema tatu kwa kiasi hicho cha fedha na wengine wanauza moja Sh 500.
Nchi hii haina viwango. Wenye daladala wakifika jioni wanatangaza nauli Sh 1,000 kwa umbali ambao gharama halisi ni Sh 300. Wenye nyumba wanapangisha kwa dola na wengine wanadai kodi ya mwaka mzima wakati hawalipi kodi hata senti tano. Wananchi wa kawaida kila mtu ananunua dola na kuhifadhi nyumbani kwake wakati dola ni za kununulia bidhaa za kimataifa nje ya nchi kwa hapa ndani tunapaswa kutumia shilingi yetu.
Sitanii, kichwa cha makala haya kinasema: “Vituo vya mafuta vinaiba kodi mchana kweupe”. Nilitangulia kusema kuwa Kenya wanatusifia Tanzania kwa kusambaza mashine za elektroniki kwa ajili ya wafanyabiashara kutolea risiti kila wanapofanya mauzo. Hii inasaidia TRA kubaini nani ameuza nini na kwa shilingi ngapi, hivyo mwisho wa kodi atakadiriwa kodi kwa usahihi.
Hapa kwetu inasikitisha. Mashine hizi zimesambazwa kila kona, lakini hazitumiki. Sisi hapa ofisini kwetu tunayo hiyo mashine. Kila siku iendayo kwa Mungu tunapeleka taarifa TRA na haigomi. Kinachonisikitisha ukienda kwenye kituo chochote cha mafuta, mara nyingi unaambiwa kuwa mashine hiyo ya tiketi za elektroniki haifanyi kazi.
Ukiuliza unaambiwa mtandao uko chini na hata madukani baadhi ya maduka nao wanatoa jibu hili. Kimsingi huu ni wizi wa mchana kweupe. Hakuna cha mashine hizi kuharibika au nini, bali wenye vituo vya mafuta wanaamua kuiba kodi za umma mchana kweupe. Wanajua wasipotoa risiti za elektroniki wananufaika.
Kisichoingia akilini kwangu ni iwapo TRA hawayaoni haya. Sheria iko wazi. Inatamka bayana kuwa mtu yeyote mashine hiyo ikiharibika inapaswa kutolewa taarifa ndani ya saa 12; na TRA watatoa mafundi wa kuitengeneza. Mimi naona hapa kinachoendelea ni dili. Wapo wamiliki wa vituo vya mafuta na maduka wenye uhusiano usio rasmi na baadhi ya maafisa wa TRA.
Hawa wananufaika na mfumo wa risiti za vitabu. Risiti hizi hazina uwezo wa kutoa kumbukumbu sahihi na ufuatiliaji wake ni mgumu. Ndo nasema wakati umefika sasa. TRA waanzishe kitengo maalumu cha kuwakagua wenye mashine hizi iwapo wanazitumia ipasavyo. Kwa kuendelea na utaratibu huu, wafanyabiashara watazidi kutunisha mifuko yao kwa gharama ya kulikondesha Taifa.