Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kahama
HATUA ya Serikali Kuu kuipatia Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, Shinyanga zaidi ya Tsh. 4.5 Bilioni, imewezesha halmashauri hiyo kukamilisha majengo yake.
Halmashauri hiyo imepanga kuhamia kwenye majengo yake yaliyopo Izengabatogilwe, Kahama mwanzoni mwa Oktoba, 2023 kutoka ilipo sasa katika Kijiji cha Ntobo A.
Kauli hiyo ilitolewa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Khamis Katimba katika kikao cha kawaida cha kila mwezi kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo tarehe 13 Septemba 2023.
“Halmashauri tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuleta fedha kwa ajili ya kumalizia jengo la utawala la halmashauri yetu ikiwa ni pamoja na matumizi mengine kama ununuzi wa fenicha za ofisi, miundombinu ya umeme, maji, TEHAMA na marekebisho madogo madogo.
“Halmashauri yetu ilipokea kiasi cha Tsh. 4.5 Bilioni ambacho kwa kiwango kikubwa, kiliongeza kasi ya kumalizia ujenzi huo,” Katimba alikieleza kikao hicho.
Akimkaribisha mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mibako Mabubu kwenye kikao hicho, alisema majengo yanayotumika sasa si makazi ya kudumu ya halmashauri hiyo.
“Hapa tulipo hayakuwa makazi ya kudumu, yalikuwa makazi ya muda wakati halmshauri ilipokuwa ikijenga majengo yake.
“Tayari majengo yamekamilika na kwa ubora unaokidhi viwango hivyo, hatuna sababu ya kuendelea kuwepo hapa wakati tunayo majengo bora,” alisema Katimba.
Kwenye kikao hicho, mwenyekiti Mabubu alimpongeza Katimba katika kusimamia kazi za halmashauri kwa wakati na ufanisi mkubwa.
“Umefaulu vigezo vyote walivyokuwa wameweka kwenye nafasi hiyo, kwani ndani ya mda mfupi alioutumikia umma wa wananchi wa Halmashauri ya Msalala, matokeo yanaonekana sambamba na miradi kutekelezwa kwa wakati.
“Waheshimiwa madiwani wanaridhishwa na kazi yake, wazabuni na watumishi wanapata stahiki zao. Kubwa zaidi mapato yanakusanywa katika kila chanzo na hivyo kupelekea halmashauri kukusanya asilimia 30 ndani ya robo ya kwanza,” alisema Mabubu.
Akiwasilisha taarifa ya fedha, muweka hazina wa halmashauri hiyo, Gordon Dinda alisema katika kipindi kuanzia Julai Mosi hadi Agosti 31, halmashauri hilo ilifanikiwa kukusanya Tsh.1,539,753,315.82 sawa na asilimia 27 ya lengo la kukusanya Tsh.5.7 Bil kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Alisema, vyanzo vyake ni kodi ya huduma, ushuru wa pamba, ada ya zabuni, ushuru wa mazao mengineyo na ushuru wa mpunga/mchele.
Akichangia hoja Diwani wa Kata ya Ikinda, Matrida Msoma alisema, wataalamu wa halmashauri hiyo wanapaswa kutumiwa mbunu mbalimbali kuhakikisha halmashauri hiyo inaongeza makusanyo yake.
Akijibu swali la makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhusu urejeshaji wa fedha za mradi wa upimaji viwanja katika kata za Isaka, Bugarama, Segese na Kakola, mkurugenzi Katimba alisema, marejesho hayaridhishi.
Katimba aliwataka watumishi ndani ya halmashauri hiyo kuwa mabalozi wa kuelezea fursa za viwanja vinavyopatikana katika halmashauri hiyo, kwani vipo barabarani na huduma muhimu kama umeme na maji kwa baadhi ya maeneo, itafika muda si mrefu.