Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anashutumiwa na vyombo vya dola kwa kauli zake zinazowachochea wananchi kutotii mamlaka za nchi na sheria za uhifadhi.
Akiwa wilayani Ngorongoro amewataka wananchi wanaohama kwa hiari kutotii mpango huo, akisema hawana sababu ya kuhamishwa hapo kupisha uhifadhi.
Sisi kwa upande wetu tunaona kuwa pamoja na nia nzuri ya kuwapo uhuru wa kisiasa nchini mwetu, masuala muhimu yanayogusa masilahi ya taifa hayapaswi kufanywa kwa mitazamo ya kisiasa.
Sote tunatambua, na ulimwengu unatambua umuhimu wa maisha ya binadamu katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, pamoja na rasilimali zinazopatikana katika eneo hilo ambazo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limelitangaza kama Eneo la Urithi wa Dunia. Dunia nzima inajua umuhimu na faida za kulinda eneo hili.
Taarifa zote za watafiti wa ndani na nje ya nchi zimebainisha wazi kuwa hatua za kupunguza idadi ya watu Ngorongoro zisipochukuliwa, urithi wote huo utakufa, maana watu na mifugo vimelilemea eneo.
Inasikitisha kuona kuwa wanasiasa badala ya kuungana na kupata majawabu kwa matatizo haya bila kuathiri wanadamu, wanyamapori na mifugo, sasa wanakuwa mstari wa mbele kuhamasisha uharibifu zaidi.
Kauli zinazohamasisha wananchi kutotii sheria za uhifadhi zinaweza kusababisha migogoro ya ardhi na kijamii katika eneo la Ngorongoro. Wananchi ambao wanaondolewa kutoka maeneo ya uhifadhi wanaweza kuhisi kutendewa ukatili, na hii inaweza kusababisha migogoro kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi.
Kauli hizi za wanasiasa zinaweza kudhoofisha utawala bora kwa kuwafanya wananchi wasitii sheria na mamlaka za nchi. Utawala bora unahitaji kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Kutozingatia sheria kunaweza kuhatarisha utawala bora na kuleta utata katika usimamizi wa rasilimali za uhifadhi.
Kutozingatia sheria za uhifadhi na kuruhusu uhamishaji wa wananchi katika maeneo ya uhifadhi kunaweza kuwa na athari kubwa kwa uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.
Kutoa kauli ambazo zinazidi kutia chumvi katika migogoro kuna athari mbaya kwa uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii. Tunatoa mwito kwa wanasiasa kutotumia ghiliba katika kuharibu mambo mazuri ambayo nchi ingependa iendelee kuwa nayo bila kujali ni chama gani kipo madarakani.
Siasa zifanywe nje ya uhifadhi, lakini pia tujifunze kama taifa kuwa na mambo tunayokubaliana wote kwa manufaa ya kujenga taifa lililo imara.