Wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemaliza mkutano wake wa Nane. Katika mkutano huu kimemchagua Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na wa Visiwani, Dk. Ali Mohamed Shein, huku Wilson Mukama aliyeingia madarakani kwa kuwapiga fitina viongozi waliomtangulia akienguliwa wadhifa huo alioutumikia kwa miezi 17 tu, na ukatibu Mkuu wa CCM ukatua kwa Abdulrahman Kinana.

Napenda kuamini harakati za uchaguzi ndani ya CCM ulizisikia msomaji, wakitajana kuwa kuna kundi lilipanga kupiga kura za Maruhani. Kwa hofu hii, ikaelezwa kuwa CCM kililazimika kubadili utaratibu wa kupiga kura na kuamua kura zipigwe mkoa kwa mkoa, badala ya kupiga kama Mkutano Mkuu, hali ambayo pengine ingazaa zahama kwa Mwenyekiti wa CCM.


Waliibuka wengine wakasema hizo zilikuwa propaganda sawa na zilizoshuhudiwa mwaka 2010, ambapo mmoja wa wanasiasa wakongwe ndani ya chama hicho alizushiwa kuwa anataka kugombea urais amg’oe madarakani Kikwete kutokana na ‘bifu’ walilonalo. Mwanasiasa waliyemtaja kuwa na nia hii si mwingine, bali yule ambaye hawakukutana barabarani; Edward Lowassa.


Hili halikutokea. Tukaanza kuzisikia kauli za kwamba Lowassa sasa alikuwa anaandaa kundi la kumg’oa Rais Kikwete kwenye uenyekiti wa Chama katika uchaguzi uliomalizika juzi, nalo halikutokea. Tukaambiwa kuwa Lowassa ameandaa kundi la kupiga kura za maruhani, nalo halikutokea. Lakini pia tukaelezwa kuwa Lowassa ametoa rushwa kila kona ya nchi hii kufanikisha ushindi wa wagombea anaowapenda yeye. Kila aliyeshindwa alisema ushindi wake umezuiwa na Lowassa.


Sitanii, baada ya yote haya mimi katika hili nikashika tama. Sikupata fursa ya kudurusu kila kitu, ila nikajaribu kujikumbusha tulipotokea kama taifa, tulikopitia chini ya uongozi wa CCM na tulipo sasa. Nikajiridhisha kuwa tayari CCM imepoteza mwelekeo. Inatekeleza kwa dhati dhambi ya kujadili na kuhukumu watu badala ya ajenda zenye tija kwa taifa hili.


CCM baada ya kushindwa kutufanyia kazi tuliyoituma, sasa inatafuta pa kuangushia matatizo yake. Wapo watu wanaoshindwa katika mbio mbalimbali, lakini mara tu baada ya mashindano kisingizio cha kwanza ni ama uwanja ulikuwa mbovu, viatu vilikuwa vinateleza au sikuusikia vizuri mlio wa ngoma ya kuondoka.


Hapo wanatafuta nafuu ya kuwafanya mashabiki wao wawaoneee huruma na kuhamishia tatizo la kushindwa kwako kwenye uwanja mbaya. Huu ndio mchezo wanaotufanyia CCM kwa makusudi kupenyeza habari za kuwataja akina Lowassa kila kona. Wanafanya hivyo kwa nia ya kuifanya jamii iwaone wao ndo wazuri na kwamba kama si akina Lowassa basi nchi hii ingekuwa ya maziwa na asali.


Kichwa cha makala haya nimesema; Chadema vaa miwani muone CCM walipoangukia. Nimesikia hata ndani ya Chadema kuna fukuto la makundi ya akina Dk. Wilbrod Slaa, Freeman Mbowe na Zitto Kabwe kila mtu ana kundi lake. Makundi haya matokeo yake ni hayo kama ya CCM na akina Samuel Sitta, Edward Lowassa na Bernard Membe.


Chadema mkiendekeza makundi haya, basi mjue mtaelekea mkondo ule ule waliopitia CCM, baadae mtaanza kutajana hadharani kuwa ama Mbowe, Slaa au Zitto ndiye anayekwamisha maendeleo ya chama hicho. Tena mmeishaanza. Vijana wenu kuna nyakati walisimama hadharani na kumtuhumu Zitto kuwa kalambishwa rushwa. Hili kwenu litakuwa shimo muwali kwa safari ya kuua matumaini ya Watanzania.


CCM kama chama kikongwe, tunafahamu kilipotutuoa. Kilikuwa kinafanya mikutano ya hadhara kila wiki na kila kona ya nchi hii kuhamasisha wananchi kujiletea maendeleo. Ajenda zilikuwa ni kilimo cha kisasa, elimu, nyumba bora ya kuishi, afya bora, mshikamano, utaifa, uzalendo, upendo, utulivu na amani. Leo dhana ya ‘mpende jirani yako kama nafsi yako,’ imebadilishwa kuwa ‘ipende familia yako kama nafsi yako’.


Sitanii, wahenga na Baba wa Taifa hawakuwa wajinga kutaka uongozi usambazwe katika nchi hii. Siyo siri kwamba mtu yeyote anapopata uongozi bila kujali kiwango cha mshahara, masilahi kidogo yanaongezeka katika familia ya kiongozi husika. Na hapo sizungumzii hata heshima inayopata familia husika. Leo tunazo familia ambazo Baba, Mama na Watoto (BMW) ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.


Niliwahi kuandika na naomba kulirudia hili, hivi leo hicho walichoshindwa kumshauri baba yao wakiwa ama sebuleni au chumbani, watawezaje kumshauri akisikie kwenye mkutano unaokaribia kuwa wa hadhara? Sasa nasema Chadema mkiamua kuchukua mkondo wa BMW msishangae wananchi wakaanza kuwaweka kundi sawa na CCM.


Enzi hizo, ilikuwa tukienda katika mikutano ya hadhara, tunasikia nyimbo hizi:


TAZAMA RAMANI

1.  Tazama ramani utaona nchi nzuri,

Yenye mito na mabonde mengi ya nafaka,

Nasema kwa Kinywa halafu kwa kufikiri,

Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzaniaaaaaaaa…,

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa,

Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha x 2

2.  Chemchem ya furaha amani nipe tumaini

Kila mara niwe kwako nikiburudika,

Nakupenda sana hata nikakusitiri,

Nitalalamika kukuacha Tanzania.

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa,

Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha x 2

.

3.  Nchi yenye azimio leeenye tuumaini,

Ndiwe peke yako mwanga wa Watanzania,

Ninakuthamini hadharani na moyoni,

Unilinde nami nikulinde hata kufa,

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa,

Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X 2

Nyimbo hizi zilikuwa zikitujengea uzalendo, kuipenda nchi yetu, kuwa na matumaini na kutupa moyo wa kutumikia nchi hadi kufa. Nyimbo za aina hii na nyingine zilikuwa zikiimbwa katika mikutano ya hadhara, na kila viongozi wa kitaifa walipotembelea mikoani, redioni na shuleni. Leo ni aibu tupu. Kwenye mikutano ya hadhara zinaibwa nyimbo hizi:

Harambeee eheee harambe mama harambeeee,

Harambeee eheee harambe mama harambeeee,

Harambe, harambe, harambe mama harambe x 2

Wapinzani, tuwashike tuwachane chane tuwatupe x 2

CCM tuwashike tuwakumbatie tuwabusu x 2

Au

Kuku kapanda baiskeli, bata kavaa laizoni x 2

Kikulacho, ehee kiunguoni mwako,

Rafiki yako, ehee adui yako x 2

Utalijua jiji, utalijua jiji,

Utalijua jijiji, utalijua jiji

Nashindwa hata kuziandika kwa ufasaha nyimbo zenyewe maana sizipendi. Hii kidogo kidogo imemomonyoa umoja wa kitaifa. Nyimbo za aina hii zimeifanya jamii ione hakuna viongozi makini. Viongozi wanapanda majukwaani kucheza “Piipiii haiwezekani.” Chadema mkienda mkono huo kudhani mnawasahaulisha wananchi matatizo yao, mtakuwa mnafanya mchezo wa kufukuza paka. Akifika mwisho wa ukuta ana utamaduni wa kugeukia anayemfukuza.


CCM hawajiulizi kwa nini vijana wengi wapo Chadema. Ni siri iliyo wazi kuwa vijana wengi wamekwenda Chadema baada ya kupewa tumaini la kusoma elimu ya juu bure. Viongozi wetu walioko madarakani walisoma bure, lakini leo wanatutukana sisi na watoto wetu kuwa eti tumekuwa wengi mno kiasi Serikali haiwezi kupata uwezo wa kutusomesha hivyo tuchangie gharama kwa njia ya mikopo au kujilipia.


Kinachonishangaza, wakati wa kupiga kura hawasemi watoto wetu ni wengi mno watajaza masanduku ya kura, hivyo kila familia ipewe idadi ya wapiga kura wachache. Tunahamasisha kuwaita hata ndugu zetu walioko ughaibuni waje kuwapigia kura. Kero ni nyingi mno. Naona safu hii inapungua nijaribu kuzitaja kwa ufupi.


Sitanii, mkulima haelewi soma kumwambia umejenga barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Mwanza na kwamba teksi inaweza kutumika, wakati yeye kahawa, katani, korosho, pamba, ufuta, ulezi au mahindi yake hayana soko. Huyu ukimwambia CCM Oyeee, hachelewi kukwambia ‘Ziiiiiiii.’


Kama CCM walivyogusia wenyewe, kero ya nyumba za kupanga wenye nyumba kudai kodi ya mwaka wakati tunapata mshahara mara moja kwa mwezi. Wamiliki wa shule binafsi kila wakiamka asubuhi wanapandisha ada.


Kuna shule za msingi sasa zina ada kubwa kuliko sekondari na vyuo vikuu. Foleni za barabara kwa jiji kama Dar es Salaam, ambako wakubwa walipaswa kujenga barabara za maghorofa nazo zinakipunguzia chama umaarufu.


Je, CCM itafanyaje kujiepusha na haya? Inachoweza kufanya ni kukata mshipa wa aibu, ikaomba ushauri kwa Dk. Wilbrod Slaaa jinsi ya kupunguza bei ya saruji, ada za shule, mabati na gharama nyingine za maisha, kisha wananchi wataiwekea ‘drip’ au kuamua kuiondoa na kupeleka mwili ‘mortuary’.


Chadema wakivaa miwani na kuyaona haya, njia ya Ikulu haina hata kokwa la kuwazuia.