Vijana waliongia baada ya wale wa kwanza walipewa majina mbalimbali, maana kazi yao kubwa ilikuwa kujenga Taifa na si kuziba nafasi katika Jeshi la Ulinzi. Novemba 1964 waliingia vijana zaidi ya 400 na hawa waliitwa “Mkupuo Maendeleo” (Operation Maendeleo). Ndiyo hasa waliofungua kambi mbalimbali za uzalishaji mali katika JKT.
Nakumbuka Chief Guide Dismas Msilu (sasa ni Brigedia Jenerali mstaafu), alikuwa kiongozi wa kwanza kufungua kambi ya Ruvu mapema mwaka 1964 na baadaye kambi ya Nachingwea, Desemba 1964 wakati mwasisi mwenzake wa JKT, Chief Guide Athman Msonge (sasa ni marehemu Brigadia Jenerali Msonge), alifungua kambi la Umoja wa Vijana pale Kinondoni (Kinondoni Youth Camp). Hadi leo bado ipo kama kituo cha UVCCM.
Hii ilikuwa kambi ya vijana kwa kusaidia kujenga nyumba bora za kisasa kwa wananchi wa Dar es Salaam (tukiita Operation Kubomoa Nyumba za Makuti).
“Operation Maendeleo” ilitoa viongozi kadhaa waliofikia uongozi wa juu katika kambi za JKT, mathalani Kanali Agustino Sanga (alikuwa Mkuu wa Kambi Nachingwea, Msange na Mgulani; Meja Oddo alikuwa Makao Makuu na Mkuu wa Kikosi cha Mgambo kule Tanga. Asst. Master Triphon Kilosa alikuwa Mkuu wa Kambi kule Bulombora Kigoma.
Mei 15, 1965 katika Mkutano wa Umoja wa Vijana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TANU na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Nyerere katika Ukumbi wa Arnautoglu, alielezea umuhimu wa JKT kwa vijana wote wa nchi hii.
Alisema ni mahali pekee panapowezesha vijana wote kujengeka kitaifa ili kupata Taifa moja la Tanzania. Akasema kuwa JKT ni kama chungu au tanuri kubwa ambamo vijana wa tabia mbalimbali wa viwango tofauti vya elimu, wa kutoka makabila mbalimbali ya nchi yetu wanapikwa na kuundwa kuwa vijana wa TAIFA MOJA lenye nguvu, tabia moja na mwenendo sawa.
Alitumia maneno “NS (National Services) is a molding pot”. Basi, chombo muhimu namna hii ndicho cha kuwatayarisha vijana kuwa wazalendo. Bila chombo kama hiki uzalendo hauwezi kujengeka. Kuanzia hapo kauli ile ya Mwalimu ilianza kutafsiriwa kwa vitendo. Moja ya tafsiri zile ilikuwa kufungua makambi mapya mikoani.
Mwaka 1965 kadri vijana walivyoingia kwa mikupuo (intakes) mbalimbali ndivyo makambi ya mikoa (Regional Camps) yavyozidi kufunguliwa. Mwaka 1965 zilifunguliwa kambi za Makutupora (Dodoma), Bulombora (Kigoma) na Oljoro Farming (Arusha) na Nyatwali (Mara). Mwaka 1966 zilifunguliwa kambi za Mkuyu Handeni (Tanga) na Kitai iliyopo Songea (Ruvuma) na Rwamkoma (Mara). Rwamkoma ilifunguliwa baada ya kufungwa Kambi ya Nyatwali.
Aidha, katika kutafsiri kivitendo maelezo hayo ya Rais kwa vijana, Mkoa wa Arusha chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Mzee Mwakang’ata, waheshimiwa wabunge akina Ole Kanchela na Edward Moringe Sokoine wakahamasisha vijana wa Kimaasai na Wamang’ati kujiunga JKT Mgulani. Si hivyo tu, bali Serikali iliandaa mabadiliko ya sheria ile iliyoanzishja JKT ya Na. 16 ya 1964 ukaandaliwa Waraka wa Serikali Na. 2 wa mwaka 1966 ili kuboresha JKT.
Kamati maalumu ya wataalamu kutoka JWTZ, JKT, Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Kivukoni na TYL Makao Mkuu wakandaa mapendekezo ya kuboresha JKT; Mwenyekiti akiwa Waziri Mkuu Rashid Kawawa.
Matokeo ya mapendekezo yale yaliwezesha kutungwa kwa Sheria mpya Na. 64 ya mwaka 1966. Katika sheria ile uliainishwa utaratibu wa kujiunga JKT. Makundi matatu ya vijana wa kujiunga JKT yaliainishwa kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati ile. Mpango mzima uliitwa HUDUMA YA TAIFA na kwa kuanzia mpango ulihusisha watu wafuatao:-
– Wanaohitimu kidato cha sita
– Waliohitimu chuo kikuu; pamoja na wale ambao wamewahi kufuzu chuo kikuu chochote.
– Wahitimu katika baadhi ya vyuo vya utaalamu.
– Watu wote ambao wamepata kazi kwa njia ya Huduma ya Taifa.
Utaratibu mpya katika sheria hii ulitoa nafasi kwa watu ambao watapendelea kujitolea kufanya mazoezi ya kawaida ya huduma ya Taifa (wengi wa hawa ni watu wazima). Basi, JKT ilikuwa na makundi matatu kwa majina haya:-
1) Wa kujitolea (volunteers – elimu ya msingi)
2) Wa mujibu wa sheria (compulsory – wasomi wote)
3) Watu wazima (mature age – wazee waombaji kulitumikia Taifa)
Kwa utaratibu huo, JKT ilijiandaa kupanua nafasi katika shule ya mafunzo ya awali Mgulani. Ndipo zikafunguliwa shule nyingine mbili – moja Mafinga Iringa (1967) nyingine Ruvu, Pwani (1967). Hivyo kwa kuanzia ziliandaliwa shule tatu kutoka Mgulani, Ruvu na Mafinga.
Jambo hili la kuwaita wasomi kujiunga katika kambi za JKT liliwakera sana wasomi mwaka 1966 na wakaamua kulipinga kwa maandamano kwenda Ikulu Oktoba 22, 1966. Wakibeba mabango na risala yao yenye maneno makali kama vile “…afadhali enzi ya mkoloni kuliko leo hii”, au tukilazimishwa, basi miili yetu itakwenda huko makambini, lakini mioyo yetu ng’o haitakuwa huko”.
Mwalimu alistushwa mno na maandamano yale. Alikasirishwa na matamshi yao na akaamua mambo mawili. Moja, kuwatimua wale wote walioandamana na kuwarudisha makwao mara moja. Pili, aliamua kupunguza mshahara wake kwa Sh. 1,000 na mishahara ya mawaziri wake kama alama ya kujitolea kwake kwa huduma ya Taifa hili.
Oktoba 23, 1966 majeshi yote JWTZ, Polisi, Magereza, JKT, TYL na wote wenye usongo na uzalendo kwa nchi hii walifanya maandamano makubwa pale ofisi ya TANU, Lumumba, Dar es Salaam. Mwalimu aliwahutubia waandamanaji wote na kupitia kwao, Taifa zima.
Baadhi ya maneno yale yalikuwa haya namnukuu, “… Wananchi, jana tumefukuza wanafunzi wapatao 393 kutoka vyuo mbalimbali vya Dar es Salaam baada ya maandamano yao ya kupinga mpango wa Serikali wa National Service…” Wametoka Chuo Kikuu Mlimani, Chuo cha Ufundi hapa nyuma yenu, Chuo cha Madaktari kule Muhimbili, Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Chuo cha Biashara hapa nyuma ya Chuo cha Ufundi na wachache kutoka shule za sekondari”.
Akaendelea, “Vijana walikuja Ikulu kupinga mpango wa National service. Nataka kuwaelezeni ninyi na nchi nzima, ‘National Service’ maana yake nini. Wananchi, National Service hatukuanzisha sisi, mataifa mengi duniani yana National Service. Taifa linawaambia vijana wake. ‘Tunataka vijana mlitumikie Taifa lenu’. Taifa linadai utumishi toka kwa vijana. Linadai huduma kwa vijana na vijana wakaitikia wito huo kwenda kulihudumia Taifa kwa kazi yoyote ambayo Taifa linahitaji ifanywe.
“Kwa desturi National Service au huduma wanayoitiwa vijana hawa wa mataifa mengine haya duniani ni huduma ya kivita. Wanaitwa kwenda wakafundishwe kwa kazi ya kivita. Na wanapoitwa jinsi hiyo vijana hao wote wanafanywa sawa sawa. Mwingine labda atakuwa mwalimu mwingine labda alikuwa fundi chuma, mwingine labda ni daktari. Huyu udaktari wake kasomea miaka saba, yule ualimu kasomea miaka mitatu – kundi lile la National Service, wakishafika pale basi wote sawa. Wanakuwa askari wa kawaida, hakuna anayehesabiwa digrii, la, ijapokuwa aingie na digrii ishirini, ukishafika pale (kambini) wewe na mwingine wote ni (makuruta) private yaani askari wa chini kabisa.
“… sisi wananchi tumeanzisha National Service hapa. Vijana wale mnawaona pale (nilikuwa mmoja wa waandaaji hao) ni vijana wa National Service. Tofauti ya kweli baina ya National Service yetu na zingine ya kwetu si ya kivita, ni ya ujenzi wa Taifa. Tumewaita na kazi tutakayowapa ni ujenzi wa Taifa. Tunaona vijana wenye elimu hawaji. Waliosomea kazi maalumu hawaji, mwenye kutambua na kazi yake mahali haji tukaona hapa pana kasoro. Vipi waliokwisha tumikiwa na Taifa vizuri sana wao ndiyo hawaji kulihudumia Taifa katika National Service? Tukaligundua hilo na tumelirekebisha…” (mwisho wa kunukuu).