Wiki iliyopita, kwenye safu hii, niliandika makala kuhusu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupokea msaada dhalili wa ambulance moja kutoka kwa “Watu wa Marekani”.
Nilisema msaada huo ni fedheha kwa nchi yetu ambayo imejaliwa kuwa na rasilimali na ukwasi usio kifani. Tena basi, ni fedheha kwa chombo kama JWTZ ambacho katika hali ya kawaida tunapaswa sisi Watanzania wenyewe tuhakikishe kimairishwa bila kuendekeza utegemezi.
Baada ya makala hiyo, wasomaji wengi wamejitokeza kutoa maoni yao kupitia mtandaoni. Nimeona ni vema nikaweka maoni hayo ili wahusika wajue ni kwa kiasi gani Watanzania hawafurahishwi na hii ombaomba inayofanywa na viongozi katika Taifa letu hili tajiri.
………………
Asante kwa kuwakilisha, mwana kwetu, kweli kabisa hawaoni hata aibu, na vyote ulivyovitaja hapo ni kweli kabisa, ukisikia umasikini usiuvalie koti ni huu. Taifa hili siyo masikini, lina kila rasilimali na tumejaliwa kuwa na rasilimali nyingi, lakini tuna ujinga ndani yake. hatutumii akili kunufaika na raslimali zetu, bali tumejaa, ujinga na ufisadi ukichanganya na ufisadi wa mawazo.
………
Umesahau msaada wa mipira na baiskeli vilivyopokelewa Ikulu? Semebuse ambulance!
………..
Zawadi ni zawadi tu, kama hiyo ambulance moja inatosha. Watanzania ni wavivu kimawazo na bado tunaishi miaka 20 iliyopita. Utajiri tunao, lakini hatutaki kufanya kazi kwa bidii. Rais ndiye anaeongoza kuomba misaada nje wakati anatakiwa kuwahamasisha wananchi wafanye bidii.
Kwa herufi kubwa…tuko kama mateja!
……….
Kwanza, kama Rais mwenyewe anafunga safari ya kwenda kuomba neti, itakuwa hao walioomba ambulance? Pili, huoni hata bungeni mawaziri wanavyojiaminisha kwamba wageni wakipewa ardhi yetu ndiyo njaa hatutaiona kwetu Tanzania?
Mimi nahisi sisi ngozi nyeusi tuna matatizo!
Kuna kisa cha mzungu mmoja kule Wilaya ya Bunda alichimba kisima cha maji kijijini kwa gharama ya Sh milioni 20 kama msaada; siku ya uzinduzi akaja mkuu wa wilaya kuzindua akiwa ndani VX kali, kwa ajabu ya mzungu yule, akamsifia mheshimiwa DC kwamba gari lake kali, na akamuuliza lina-cost kiasi gani? DC akamjibu kwamba kama Sh milioni 100 hivi. Mzungu akamwambia hiyo ingechimba visima vingine vitano kwenye vijiji vya jirani! Lakini DC wala hakuonekana kusononeka!
Mwaka 2006 Ayoub Ryoba aliandika kwenye gazeti la Citizen makala kuhusu serikali yetu kuagiza ma-Land Cruiser VXs na GXs kutoka Japan; na Japan kama asante huwa wanatujengea matundu ya choo kwenye shule zetu za msingi kama pale Tabata!
Je, kuagiza VX na GX zaidi ya 500 kwa mkupuo kutoka Japan huku tukijengewa matundu ya choo siyo fedheha kuliko hiyo ya ambulance? Miafrika tuna matatizo sana popote tulipo!
…..
Kwi kwi kwi (kicheko)…Angalau mtu kakiona nilicho kiona na kujiuliza.
………..
Magufuli alimwambia Kikwete aongeze u-Matonya (ombaomba) huko nje, ili nchi ipate maendeleo. Kuna msemo kuwa kwenye wingi wa maji, ni mjinga tu atalalamika kwa kiu. Tanzania tunalalamika kwa kiu (umasikini) wakati tunaloana kwa maji (rasilimali na utajiri lukuki).
Ajabu, katika mpangilio wa picha za leo, inayofuatia hapa chini ni ya watoto ‘wanatafuta’ kitoweo kwa kubahatisha samaki ajilete mwenyewe. Ndiyo fikra na mawazo yetu kama nchi. Ziwa lote hilo, tumesimama ufukoni tunasubiri kubahatisha kupata samaki badala ya kufikiria kuingia katikati na kuwasaka hao samaki.
……..
Toka lini Magaharibi wakatusaidia kwenye maendeleo ya kweli ya elimu, sayansi na teknolojia? Gender (jinsi), haki sawa, ukimwi, malaria, kisima cha maji na dini ndiyo mpango wenyewe!
……….
Kaka Jackton naungana nawe, ni kweli misaada mingine ni fedheha, lakini kuna wakati ambassador (mabalozi) wana-donate i mean just to give back to the community, serikali yetu inaweza mambo mengi tu, tatizo ni watendaji wa katikati.
Nakupa mfano baadhi ya halmashauri mwisho wa mwaka hurudisha fedha Hazina, huu ni ukweli mtupu na hizo fedha nakukuakishia ndiyo watu wajanja huwa wanaziiba- hazirudi Hazina na bado utakuta kwenye hiyo hiyo halmashauri wanafunzi hawana madawati, huduma mbovu za maji, huduma mbovu za afya. Kuna tatizo la watu kutofikiria mbali. Fedha za migodi si unajua wamiliki kaka Serikali inapata kidogo sana pale, nafikiri unatambua hamna mgodi wa serikali, mikataba mibovu imewapa nguvu zaidi wageni…
…….
Kweli kwenye miti hakuna wajenzi. Na uvivu wa kufikiri ni mwiba ukuchomao. Waafrika tuna uvivu wa kufikiri. Mungu ametujalia kila kitu. Kuna mmiliki mmoja wa hoteli pale Zanzibar (Mtaliano) niliwahi kufikia hotelini hapo siku kama tano. Tulianza kuzoeana na kumsifia kwa juhudi za kutengeneza hoteli kama hiyo iliyosheheni kila sifa.
Aliniambia mahali pa zuri pa kufanya biashara bila kubughudhiwa hapa duniani, ni Tanzania pekee. Aliongeza kwamba amezunguka sehemu nyingi duniani -mfano Afrika Kusini- hapakumfaa kabisaa! Akaenda Kenya, huko balaa tupu, akaingia Uganda hakuweza kuchuma. Akaenda Naigeria wakam-Nigeria (wakamtapeli), akaamua kuiingia nchi unayoweza kumwita hata waziri kwenye hoteli uliyofikia ukamnunulia ka-bia na ka-nyama choma akakupa kila utajiri unaotaka. Ukweli ni aibu tena kubwa.
Nikamshauri sasa atafute mke wa Kitanzania mwenye akili za kufikiri ili azae watoto watakaorithi huo utajiri! Alinipa hicho kibarua ambacho bado nakifanya. Mimi tayari nimeshaolewa. Labda ningejitolea.
Wadau hii ndiyo inayompelekea Rais kutalii kama mnavyoita. Inafikia hatua tumwonee huruma huyu Rais. Maana kama watu anaotuongoza ndiyo sisi hata tuliopewa dhamana ya madaraka tunashindwa kumsaidia atafanya nini baba wa taifa la watu zaidi ya milioni 40? Sina maana aendelee kuomba omba, bali ni sisi wenyewe tunaomtuma akaombe kuanzia viongozi hadi wewe mdau!
Angalia nchi zingine duniani hadi vyanzo vya maji unatembea maili kibao huoni mto, huoni bahari wala ziwa, lakini hawajawahi kukosa maji wala umeme kukatika. Misaada mingine ni siri ya watoa misaada ili waendelee na malengo yao.
Kaulimbiu kwa pamoja tutafakari na tuikatae tuone kama watapona hao wanaoutupatia. Natambua kuna misaada mingine isyoepukika hata mataifa makubwa hufikia hatua huomba. Lakini imefikia kwa Tanzania kujitafakari. Tuna kila sababu ya kutumia rasilimali zetu zinazoibiwa kila kukicha. Kama viongozi wataacha tamaa ya kuwa matajiri bila kufikiri, tunaangamia. Viongozi waache anasa zisizo za msingi, kupenda makoti makubwa kumbe yamejaa chawa. Magari ya kifahari nk.
………………
1: Ninaomba hiyo ambulance irudishwe.
2. Chunguza hotuba za rais zilizo nyingi, huzungumzia kuombaomba
………
Mimi kaulimbiu yangu kwa Watanzania wote kuanzia sasa kuelekea mwaka wote ujao wa 2013 ni hii ifuatayo: Watanzania tuache kulalamika, tuondokane na nadharia na ‘siasa za michakato’ tufanye kwa vitendo, tutende, tusiendelee kubwabwaja ili kujinasua katika Lindi hili la umasikini linalotukabili kitaifa, lakini muhimu zaidi kutokomeza umasikini katika ngazi ya kaya. Usifikiri unaweza, fanya kwa vitendo; usifikiri ni rahisi kutenda, tenda kwa vitendo; usiogope kujaribu, jaribu kwa ujasiri kwamba utaweza, kwani walioweza wana nini? Kila Mtanzania ajaribu kuwa na positive thinking.
Inawezekana, hakuna kisichowezekana duniani, hususan pakiwepo na umoja wa nia ya dhati na ushirikiano wa pamoja tukitanguliza utaifa au uzalendo.
Kupitia utaifa na uzalendo hata wewe mmoja mmoja utanufaika kwa jitihada zako! Watanzania tusiwe wepesi wa kulaumu na kulalamika.
Huo ndiyo mwanzo wa kushindwa. Hakuna aliyefanikiwa duniani kwa kuanza na lawama au malalamiko kwa wenzake. Bali aliyeuchukulia upungufu uliyopo au uliojitokeza kama changamoto, kichocheo kilichoisukuma dhamira yake na kipaji chake, katika kuiokoa jamii au taifa lake. Mwanzo mzuri hapo siyo kulaumu au kulalamika, bali kupendekeza.
………..
Waungwana na wazalendo wapenda maendeleo huwa hawalalamiki kabla ya kujaribu; na hata kabla ama baada ya mafaniko hufurahia na hata kabla ya mafaniko hawakati tamaa.
Watanzania tuondokane na tabia ya mazungumzo badala ya vitendo. Hebu tujaribu kuiweka akili kama mtambo unaojiendesha. Mdau kanikumbusha kuhusu mke anayeachiwa pesa kisha kuomba sabuni kwa jirani.
Kuna wengi wa namna hiyo… anaomba nauli kwa machozi ama pesa ya kula mlo mmoja! Ukimpa mia tano kidogo, ukimpa elfu matusi kana kwamba kakukopa, ukimpa milioni anaanza kutamba tena kwa maneno ya kejeli.
Wito wangu imefikia hatua tujinyime na tuanze safari hii ndefu ya kujifunza kupitia kwa wenzetu ambao wameendelea.
Hao si kwa sababu wao Mungu kawapendelea la, bali wanafanya kazi kwa bidii na stress juu. Pesa zao ndiyo tunazitumbua hapa hapa kwetu kwa kukatwa kodi zao! Ni aibu mno na inaumiza mwenzio afanye kazi, wewe ungojee kuomba omba.
Misaada kama hiyo huwa matumizi yake hayana plan na hutupumbaza. Ni sawa na kumpa mtu pesa kila siku bila kumpa mwelekeo kisa anajua kuomba tena kwa machozi ya mamba. Hatujengi, bali tunabomoa.