Juhudi za makusudi zinahitajika haraka kunusuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupoteza mvuto na heshima mbele ya jamii.
Katika siku za karibuni, wabunge na mawaziri kadhaa wamedhihirika kupungukiwa na umakini wakati wa kuchangia na kujibu hoja mbalimbali bungeni.
Baadhi ya wabunge wamesikika wakijadili mambo yaliyo nje ya hoja zinazojadiliwa, huku wengine wakizungumza kwa jazba na kutoa kauli zisizostahili bungeni. Wengine wamekuwa wakitamka kimakosa maneno na maji ya watu na vitu.
Kwa upande mwingine, baadhi ya mawaziri wamejenga kasumba ya kujibu maswali ya wabunge kibabe, kwa sauti kali na wengine kuishia kutoa majibu yasiyokidhi maswali husika.
Kibaya zaidi, wabunge hawajaonesha umoja na mshikamano katika kutetea maslahi ya umma wa Watanzania. Mara nyingi wamekuwa wakitumia hisia za tofauti zao za kiitikadi kupingana hata pasipostahili kupingana. Wengi wamekuwa wakijadili hoja katika sura ya kuvipigia debe vyama vyao vya siasa. Wanaojitahidi kuweka kando tofauti za kiitikadi wakati wa kujadili maslahi ya wananchi ni wachache mno.
Haya yamedhihirika hata katika vikao vya mkutano wa tisa wa Bunge vilivyofanyika kati ya Oktoba 30 na Novemba 9, mwaka huu, mjini Dodoma. Ni mambo ambayo hawakutumwa na wapigakura wao.
Wakati fulani katika moja ya makala zangu za uchambuzi, nilisema wanasiasa wengi nchini ni wenye ROHO MTAKA-VITU. Ni watu wanaotafuta ‘ulaji’ wao binafsi, siyo kuwatumikia wananchi.
Ushahidi wa ninachokisema uko wazi. Wabunge wengi wamehamia Dar es Salaam siku chache baada ya kuchaguliwa. Wanatumia mishahara yao minono kujifutia umaskini, kujijenga kiuchumi na kujiboreshea maisha na familia zao, huku wapigakura wao wakiendelea ‘kukaangwa’ na matatizo lukuki majimboni.
Wengine ni vinara wa kuzungumza kwa sauti na jazba kubwa bungeni ili waonekane na kusikika kuwa wanaguswa na matatizo ya wananchi, lakini kivitendo ni butu. Kuna waliotelekeza majimbo yao kwa muda mrefu na hata wanapopigiwa simu na wapigakura wao hawapokei.
Taswira hiyo ndiyo sasa inadhihirika kwa wabunge wengi. Nia zilizowasukuma kuomba ubunge ni zaidi ya uongozi wa kuwatumikia wananchi kwa kushughulikia matatizo yanayowanyima maendeleo.
Kwa mfano, utakuta mbunge anapata ujasiri wa kupinga hoja ya mbunge mwezake ya kupinga ugawaji ardhi unaotoa kipaumbele kwa wawekezaji wa kigeni, huku wazawa wengi wakikosa ardhi kwa ajili ya shughuli za kujikimu na uzalishaji mali.
Lakini pia, utakuta mwingine anampinga mwenzake anayejenga hoja ya kuishauri Serikali, iongeze udhibiti dhidi ya tatizo la michango holela katika shule za msingi na sekondari.
Pia kuna wabunge wanaotoa hoja zisizo na mashiko (dhaifu), ilimradi tu waonekane na kusikika wamezungumza bungeni. Wengine siku zote hawachangii wala kuuliza chochote bungeni. Hii si aina ya wabunge tunaowataka.
Umakini umepungua miongoni mwa wabunge na mawaziri wetu, na kwa sababu hiyo wanaelekea kuligeuza Bunge kuwa ukumbi wa malumbano yasiyo na tija kwa wananchi waliowachagua. Wamejikita katika kutetea maslahi ya vyama vyao na wao binafsi.
Mwisho wa siku, mvuto na heshima ya wabunge, mawaziri na Bunge kwa jumla vitapukutika kwa uzembe wa wahusika kutokuwa makini katika uwakilishi wao kwa wananchi. Itakuwa aibu katika uso wa dunia.
Hata hivyo, bado wabunge hawajachelewa sana kurekebisha taswira hiyo mbaya wanayoipatia mwanya bungeni. Bado wana muda wa kujirekebisha kwa kuhakikisha wanatumia vikao vya Bunge kutafuta ufumbuzi thabiti wa matatizo yanayowakabili Watanzania.
Cha msingi ni kila mbunge na waziri kuhakikisha anakuwa makini kujadili na kujibu hoja zinazogusa maslahi ya umma. Bungeni si mahali pa kuoneshana ubabe wa kisiasa na umaarufu wa vyama vya siasa. Ni mahali pa kujadili na kutafuta maendeleo ya wananchi.
Fikra ya Hekima inaamini kwamba umakini, umoja na mshikamano wa wabunge utaimarisha heshima ya Bunge na kuwezesha upatikanaji wa ufumbuzi thabiti wa matatizo lukuki yanayoendelea kuwanyima wananchi maendeleo ya kweli.
Utaifa kwanza, itikadi baadaye.