Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo itakuwa kitovu cha upasuaji kwa njia ya matundu madogo katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa vifaa tiba vya kisasa na uwepo wa wataalam bobezi.
Prof. Janabi ameyasema hayo mapema leo alipokutana na jopo la wataalam ikiwemo madaktari bingwa bobezi, wataalam wa usingizi na ganzi pamoja na wauguzi ili kuwapongeza baada ya kushiriki kufanya upasuaji mwishoni mwa wiki wa kuondoa bandama kwa kutumia njia matundu madogo ikiwa ni mara ya kwanza upasuaji huo kufanyika nchini kwa kutumia mfumo huo ukilinganisha na njia ya kawaida iliyokuwa ikitumika hapo awali ya kufungua tumbo.
Prof. Janabi ameongeza kuwa upasuaji huu wa kutumia matundu madogo ni wa kisasa ambao humpunguzia mgonjwa muda wa kukaa hospitalini, gharama kwa mgonjwa husika na pamoja na pia mgonjwa hawi na kovu kubwa baada ya upasuaji.
“Mgonjwa anaweza kuruhusiwa siku ya kwanza au ya pili baada ya kufanyiwa upasuaji huu wa matundu madogo, unaweza kufanyiwa Jumamosi na Jumatatu ukaingia kazini kama wewe ni mfanyakazi kuendelea na majukumu yako ya kila siku na hata watu wasijue kama umefanyiwa upasuaji kwa kuwa hutakuwa na kovu kubwa” amesema Prof. Janabi.
Kwa upande wake daktari bingwa Mlmbobezi wa magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Viungo vinavyohusiana na Mfumo wa chakula, Dkt. Hamis Katembo amesema mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kuondoa bandama kwa njia ya matundu mwishoni mwa wiki aliruhusiwa siku moja baada ya huduma hiyo na anaendelea vizuri na majukumu yake ya kila siku.
Kwa sasa MNH inatoa huduma ya uchunguzi kwa njia ya matundu madogo pamoja na upasuaji ikiwemo kuondoa kidole tumbo, kuondoa makovu ya ndani baada ya upasuaji, kuondoa utumbo mpana, kuondoa kizazi chenye shida, kuondoa ngiri kokoto, kutatua changamoto za kumeza na huduma nyinginezo.