Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi- Dar es salaam.
Jeshi la Polisi limewakumbusha wananchi kushiriki katika maswala ya kijamii ikiwa ni Pamoja na kuyakumbuka makundi maalum ya wahitaji yaliyopo katika jamii inayowazunguka ili kujenga ustawi katika Jamii ya watanzania.
Hayo yamebainishwa na mrakibu msaidizi wa Polisi ASP Sinasubi Serungwi ambae ni mkufunzi kutoka chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) ambapo amesema kuwa jamii inapaswa kushiriki kutoa mahitaji katika vituo na makundi ya wahitaji.
Sinasubi ameongeza kuwa kituo hicho kinahitaji sana misaada mbalimbali ambapo amewaomba wananchi kufika na kuwafariji Watoto hao huku akibainisha kuwa wamefika katika kituo hicho ikiwa ni sehemu ya sala na majitoleo yao katika umoja wa madhehebu ya kikristu kutoka chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA).
Mkaguzi wa Polisi INSP Paul Bundala amewaomba wananchi kuendelea kushiriki na kufika katika vituo vya kulea watu wenye uhitaji na kutoa misaada kwa makundi hayo maalum katika jamii ili kufanya wajione kama makundi mengine katika jamii.
Mkuu wa kituo cha Udiakonia cha kilutheri Mtoni Dayosisi ya Mashariki na Pwani Bi Winfrida Malumbo amewashukuru maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka chuop cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) kwa kuonyesha upendo kwa kituo hicho ambacho kinalea Watoto wenye uhitaji maalum.
Sambamba na hilo mwanafunzi wa kozi ya uofisa Rebaca Mwakibibi ameushukuru uongozi wa chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) kwa kuwapa kibari cha kushiriki na kutoa misaada yao katika kituo hicho ambacho huku akibainisha kuwa wao ni Polisi lakini bado ni sehemu ya Jamii na waliona vyema kufika nakutoa msaada wao alisema Mwakibibi.