Na Mwandishi Wetu. JamhuriMedia
Serikali ya Saudi Arabia itasaidia na kusimamia matibabu ya kuwatenganisha watoto waliozaliwa wakiwa wameungana Hussen na Hassan wenye umri wa mwaka mmoja na miezi 11 wakazi wa Mkoa wa Tabora ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akiagana na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Mh. Fahad Alharbi ambaye alifika MNH kwa lengo la kuwajulia hali na kuwaaga watoto hao wanaotegemewa kuondoka Tanzania Agosti 23 2023 kwa ndege maalumu ya Serikali ya Saudi Arabia, kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha.
Prof. Janabi amesema kwamba MNH ina uwezo wa kufanya upasuaji wa aina hiyo kwa kuwa ina miundombinu na wataalamu iliyojitosheleza ila kutokana namna watoto hao walivyoungana inahitaji utaalamu zaidi
“Tumekuwa na watoto hawa kwa miezi 11 wameungana kwenye nyonga, kifua na wana miguu mitatu, upasuaji kuwatenganisha ni mkubwa zaidi hivyo kesho timu ya wataalamu wa MNH ikijumuisha madaktari wa upasuaji na wauguzi itaondoka na watoto hawa kuelekea Saudi Arabiakwa ajili ya upasuaji”
Aidha Prof. Janabi ameshukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa msaada huo ambao utasaidia kuwarejesha watoto hao katika maisha ya kawaida.
Kwa Upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa MNH, Dkt. Zaitun Bhokhary amesema kuwa watoto hao walipokelewa MNH wakiwa na umri wa wiki mbili na walikuwa na changamoto mbalimbali za kiafya ambapo wamepatiwa matibabu na kutuzwa hadi kufikia hatua ya kupelekwa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya upasuaji huo.
“Kama ambavyo Profesa amesema, hawa watoto wameungana sehemu kubwa (complex conjoined twins) hivyo upasuaji wake utahitaji utaalamu zaidi” amesema Dkt. Zaitun
Dkt. Zaituni amesema wataalamu wa MNH watakaoambatana na watoto hao nchini Saudi Arabia wataruhusiwa kushiriki katika upasuaji na matibabu jambo ambalo litasaidia kuwajengea uwezo wataalamu hao.