Kufuatia jitihada zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo ubunifu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya “Tanzania the Royal Tour” ambayo imetangaza nchi ndani na nje ya nchi kwa kiasi kikubwa, Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imejipanga kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uhifadhi, utalii na ukusanyaji maduhuli.

Juhudi zilizofanyika zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia ambapo hadi kufikia Juni 2023 jumla ya watalii 242,824 walitembelea vivutio hivyo.

Kamishina wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos ametoa kauli hiyo leo Agosti 16, 2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanahabari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TFS na muelekeo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Profesa Santos amesema Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 60.8 ukilinganisha na watalii 152,002 waliotembelea vivutio hivyo kwa kipindi hicho kwa mwaka 2021.

“Jumla ya Shilingi 1,368,940,965 zilikusanywa ikilinganishwa na Shilingi 603,311,740 zilizokusanywa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la Asilimia 126.9.” – Profesa Santos.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TFS na mwelekeo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 leo Agosti 16, 2023 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma


Amesema kuwa takwimu hizo zinaweka rekodi mpya kwani Wakala haukuwahi kufikia malengo haya hapo kabla.

Profesa Santos pia ameeleza kuwa Katika kipindi cha mwaka jana pia TFS ilipewa fedha kiasi cha shilingi Bilioni nne kutoka sehemu ya fedha alizotoa Mheshimiwa Rais kuboresha uhifadhi na shughuli za utalii katika misitu.

TFS Imekamilisha kwa ufanisi ujenzi wa malango 5 katika hifadhi 5, Ujenzi wa barabara urefu km 97 na njia za kutembea kwa miguu kilomita 190.5 katika hifadhi 11.

Kupitia mpango kazi wa ndani wa taasisi TFS imeendeleza vivutio vya utalii wa kiikolojia na kiutamaduni kwa kukarabati kilomita 231.7 za njia za watalii na kilomita 643.54 za barabara za msituni; na kuandaa ramani za vivutio vya kiikolojia katika misitu ya hifadhi.

Wakala umekamilisha ujenzi wa hosteli mbili moja katika msitu wa Wino, Songea na nyingine katika msitu wa SaoHill, Mafinga Iringa na kukarabati hosteli moja katika hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.

Aidha, makambi sita (6) ya watalii katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Kilombero, Magamba na Mlima Hanang yamekamilishwa. Ujenzi wa banda 1 la kupumzika watalii, mageti matatu (3) na mabango 8 katika vituo vya Michoro ya Miambani Kolo – Kondoa na Magofu ya Tongoni – Tanga. Pia, utengenezaji wa benchi 8, meza 3 umefanyika katika Shamba la Miti West Kilimanjaro na pia miundombinu mingine mingi kuwezesha utalii katika misitu mbalimbali.

Pia Profesa Santos amesema Wakala umeendelea kutangaza vivutio vya utalii ikolojia, utamaduni pamoja na uhifadhi wa rasilimali za misitu kupitia maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ikiwemo Sabasaba, Nanenane, Tanga Trade Fair, International Tourism Expo Japan 2022, East Africa International Tourism Expo, S!TE na 2022 World Cup.

Hata hivyo Wakala kwa kushirikiana na wadau uliandaa mashindano ya utalii maarufu kama West Kili Forest Tour Challenge, Bata Msituni Festival, na Sao Hill Forest Rally.