Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika Vyama vya Ushirika lengo likiwa ni kubaini uzingatiwaji wa matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayohusiana na utendaji wa Vyama vya Ushirika.

Hayo yamesemwa leo Agosti 11,2023 jijini hapa na Mrajisi wa vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege Wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi na Mpango was kuhimarisha Ushirika kwa Mwaka 2923/24.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023 hadi kufikia Juni, 2023 TCDC ilifanya ukaguzi wa jumla ya Vyama vya Ushirika 4,712 kati ya vyama 7,300 vya ushirika kupitia Ofisi ya Tume Makao Makuu na Ofisi za Warajis Wasaidizi wa Mikoa.

“Matokeo ya kaguzi hizo yalionesha kuwepo kwa mapungufu katika utendaji wa Vyama vya Ushirika hususan maeneo ya uandishi wa vitabu, urasimishaji wa mali za Vyama, utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu nyingine za Vyama, uzingatiaji wa miongozo ya Mrajis, na madeni ya muda mrefu katika taasisi za kifedha,” Amesema.

Kuhusu hali ya upatikanaji na usambazaji wa pembejeo alisema katika kuhakikisha kuwa wakulima na wanachama wa Vyama vya Ushirika wanahudumiwa kwa kusogezewa huduma karibu, Vyama vya ushirika vimekuwa vikiratibu upatikanaji pamoja na usambazaji wa pembejeo za kilimo.

“Hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2023, jumla ya shilingi 449,922,623,196 (Shilingi 449.92 Bilioni) zilitumika kunununua pembejeo za kilimo kupitia Vyama vya Ushirika nchini kwa ajili ya wakulima kwa mazao mbalimbali,” Amesema .

Amesema Mbolea iliyonunuliwa na kusambazwa kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika ni Tani 1,266,435 yenye thamani ya 227,983,187,800 (Shillingi 227.98 Bilioni).

Amesema upatikanaji wa huduma za ugani kupitia Vyama vya UshirikaTume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika kuhusu umuhimu wa upatinakaji wa huduma za ugani na pembejeo kwa wanachama kwa wakati.

Hadi sasa, Vyama vikuu vya Ushirika vimeajiri maafisa ugani 175 ambao wameendeleea kutoa huduma za ugani kwa wakulima katika mazao ya Tumbaku, Korosho, Pamba na Kahawa.

Amebainisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika imelenga kwenye Kuimarisha Maendeleo ya Ushirika ambapo Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo inahusisha Kamisheni, Menejimenti na Watumishi wengine, imejipanga katika mwaka 2023/2024 kutekeleza maeneo saba (7) ya Kimkakati yatakayolenga kufikia Kipaumbele hicho.