Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya

Makamu wa Rais,Dk. Philip Mpango, ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa pamoja na Wizara ya Fedha na
Mipango, Mamlaka ya Mapato (TRA) na kupata ufumbuzi wa haraka kuhusu tozo mbalimbali za vifungashio vinavyotumika katika bidhaa zinazozalishwa na wasindikaji na wajasiriamali wadogo nchini.

“Wasindikaji, wazalishaji na wajasiriamali wadogo ni kiungo muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu, hivyo ni vizuri tukawajengea mazingira bora ya kufanya shughuli kwa kuwaondolea changamoto zinazowakabili, ikiwamo ya tozo za vifungashio wanavyotumia kwa bidhaa zao kabla ya kufikishwa sokoni,” amesema Dk.Mpango mwishoni mwa wiki.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wakati alipozindua kiwanda cha kisasa cha kusindika mboga za majani, matunda na vikaushio cha Mbeya Food Park kilichopo eneo la Iyela, jijini Mbeya ambacho ujenzi wake umegharimu euro 663,071 sawa na fedha za Tanzania 1,719,582,174.

Fedha za ujenzi wa kiwanda hicho ni msaada kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ufadhili wa Programu ya AGRI-CONNECT, ikijumuisha mradi wa Kilimo Bora kwa Wanawake na Vijana (KIBOWAVI) kupitia Shirika la Kimataifa la Uswisi la HELVETAS pamoja na washirika wake.

Mchanganuo wa gharama za ujenzi huo ni pamoja na jengo la kiwanda Sh bilioni 1.33, mashine za usindikaji Sh milioni 309; vikaushio na kisima Sh milioni 77.55.

Katika maelekezo yake, Dk. Mpango amewataka wadau wanaohusika na changamoto hiyo ya vifungashio kukaa pamoja na na kutafuta ufumbuzi wake kabla ya mwaka wa fedha 2024/2025 (bajeti ijayo) ambapo Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, ambaye alikuwapo katika uzinduzi aliridhia maagizo hayo.

Dk. Mpango pia amewataka wasindikaji na wajasiriamali kusindika bidhaa zenye ubora unaotakiwa kitaifa na kimataifa ili kujali afya za watumiaji na walaji, pia kukubalika na kuleta ushindani katika masoko ya kimataifa, hasa nchi jirani zinazoizunguka Tanzania.

“Kiwanda hiki pia ni fursa kwa vijana wetu wa vyuo vya kati na vyuo vikuu kuja kujifunza kwa vitendo fani mbalimbali hivyo nitoe wito kwa mamlaka zote hasa Shirika la Viwango (TBS) kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa hapa viwango vyake vinathibitishwa haraka ili zifike sokoni kwa wakati,” anasisitiza Dk. Mpango.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, akipata maelezokutoka kwa Mkurugenzi wa Mradi Kilimo Bora kwa Wanawake na Vijana (KIBOWAVI), Daniel Kalimbiy, kuhusu bidhaa zinazozalishwa na kiwanda cha Mbeya Food Park wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho wiki iliyopita. 

Changamoto ya vifungashio

Awali akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda hicho, Mkurugenzi wa Mradi wa Kilimo Bora kwa Wanawake na Vijana (KIBOWAVI), Daniel Kalimbiya, anaeleza kuwa wakulima, wasindikaji na wajasiriamali wanakabiliwa na
kodi kubwa kwenye vifungashio vya bidhaa iliyosindikwa kuongezwa thamani, hivyo kusababisha gharama za uzalishaji kuwa kubwa, kwa sababu ya uhaba na bei ya vifungashio kuwa ghali.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais, tunaomba kuondolewa, msamaha au kupuguzwa kwa kodi/VAT iwe 5% ili kiwanda kiweze kusimama imara, hasa miaka miwili ya mwanzo.

Kwa mfano, Sacheti inayohitajika sana karibia kwenye bidhaa nyingi zinazozalishwa hapa kiwandani, bei ya chini ya kuchapisha au kuzalisha ni kilo 500 za Sacheti na kila kilo ni kati ya Sh 12,000 hadi Sh 15,000,” anasema Kalimbiya.

Mkurugenzi huyo anaongeza: “Gharama hizo ni bila ‘moulid’ yake ambayo ni Sh milioni 7 kutoka kwa Omary Packaging hapa nchini Tanzania, na hakuna wengine hadi mtu aagize nje ya nchi na kianzio ni kilo laki moja na kila kilo ni kati ya dola 2.5 hadi 2.7, gharama mbazo si rahisi kuzimudu.”

Kalimbiya anaongeza kuwa changamoto nyingine inayowakabili wakulima, wasindikaji na wajasiriamali ni mitaji ya kuweza kununua mazao kwa wingi wakati wa msimu wa mavuno, kwa kuwa mazao ya bustani hupatikana kwa msimu.

“Tunaomba taasisi za fedha hasa benki zilizopata pesa kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank) kwa ajili ya kuwakopesha wanawake na vijana wajasiriamali ili waweze kuja hapa kiwandani kuwakopesha hawa wanawake na vijana wajasiramali/SMEs wasindikaji waliopo kwenye kiwanda hiki cha Mbeya (MFP) ili waweze kukua zaidi kwa kuzalisha malighafi nyingi kwa ajili ya soko la ndani na nje,” anasema.

Malengo ya kiwanda

Kwa mujibu wa Kalimbiya, miongoni mwa malengo ya kiwanda hicho ni kuondoa moja ya kwa moja changamoto ya upotevu mkubwa wa mazao baada ya mavuno, ukosefu au upungufu wa maeneo safi na salama ya kusindika bidhaa zao, wengi wanasindikia bidhaa nyumbani, hivyo kukosa nembo ya ubora, hivyo kusababisha kushindwa kukidhi vigezo vya masoko mbalimbali yakiwamo ya ndani na nje ya nchi na yote hayo kusababisha mkulima au msindikaji kushindwa kunufaika zaidi kwa kujipatia kipato kikubwa.

“HELVETAS na wadau wake TAFOPA, CODERT na ADP Mbozi kupitia mradi wa KIBOWAVI unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya Programu ya AGRI-CONNECT walipanga kujenga viwanda viwili vya kuongeza thamani mazao ya bustani (mboga za majani, matunda na viungo) ili kuwasaidia wakulima na wasindikaji wadogo na kati kutatua changamoto hizo,” anasema.

Kiwanda hicho kitatoa ajira za kudumu na za muda kwa wanawake na vijana zaidi ya 500, pia wanawake na vijana kati ya 7,000 hadi 10,000 kila mwaka.

Watanufaika na mafunzo, huduma ya usindikaji na kuongeza thamani mazao ili kujipatia kipato zaidi.
Aidha, wasindikaji na wajasiriamali watazalisha bidhaa zao kwa wingi na kiwango cha juu, hivyo kuboresha na kupanua biashara zao, kuwa na mtandao mrefu wa masoko na kuimarisha mahusiano kati ya serikali na sekta binafsi, zikiwamo benki ili kuweza kuwakopesha. Kwa sasa benki haziwakopeshi kwa sababu hawana maeneo rasmi ya kusindika mazao yao.

Mradi wa KIBOWAVI peke yake una thamani ya euro milioni tano ambapo Umoja wa Ulaya ulichangia asilimia 90 (euro 4,500,000) na HELVETAS na washirika wake walichangia euro 500,000.

Mradi huu unatekelezwa katika halmashauri 11 kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi.

Kupitia Kibowavi, jumla ya wakulima na wasindikaji 21,334 (wanawake 12,801; vijana 8,533) wamenufaika na mafunzo ya mbinu bora za kilimo, elimu ya lishe, elimu ya biashara na usimamizi wa fedha, elimu ya jinsi na jinsia, mafunzo ya kuzuia upotevu wakati na baada ya mavuno na kuongeza thamani mazao, ujenzi wa miundombinu kama vile vituo 11
vya mafunzo kwa wakulima.

Please follow and like us:
Pin Share