Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Agosti 8, 2023 ameongoza mamia ya waombolezaji katika viwanja vya Golf Lugalo kuaga miili ya watu watatu (3) waliofariki kufuatia ajali ya gari iliyotokea Agosti 3, 2023 eneo la Mbwewe Pwani

RC Chalamila akitoa salamu za Serikali amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesikitishwa sana na taarifa ya vifo hivyo na ametoa pole kwa familia Ndugu Jamaa na marafiki kufuatia misiba hiyo huku akiwaomba kuwa na uvumilivu katika Kipindi hiki kigumu.

Aidha RC Chalamila amesema Serikali itatoa mkono wa pole kwa kila familia iliyofikwa na misiba hiyo siku ya kesho nyumbani kwa familia pia amesema Rais Dkt Samia amemuagiza kutoa maelekezo Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwapatia msamaha wa matibabu Baba na Mama mzazi wa wafiwa hao ambao ni wazee katika kipindi chote watakachohitaji matibabu katika Hospitali hiyo.

Hata hivyo Chalamila amesema namna pekee ya kuwaenzi marehemu hao ni kuonyesha upendo na kuwahudumia wazazi na watoto wao kama walivyokuwa wakihudumiwa na marehemu hao enzi za uhai wao. ” Kifo ni mali ya Mungu, Machozi yanayotutoka leo yakawe tija kwa familia” Alisema RC Chalamila

Ifahamike kuwa kufuatia ajali hiyo iliyotokea eneo la Mbwewe Pwani imepoteza ndugu wa familia moja wanne (4) ambao walikua wakisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Moshi kwenye msiba wa mpendwa wao, ambapo miili ya Sia, Diana na Norah inatarajiwa kupumzishwa katika makaburi ya Kondo Ununio Wilaya ya Kinondoni.

Please follow and like us:
Pin Share