Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi na wataalamu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa waweke kipaumbele katika kuendeleza vijana ili washiriki kikamilifu kwenye shughuli za kuinua uchumi na kuwapatia ujuzi na mbinu za ujasiriamali.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza kila mkoa uandae mpango mahsusi wa kuhamasisha vijana kufanya shughuli zenye staha na kuwavutia vijana wengi kushiriki shughuli za kiuchumi, Mkoa wa Dodoma umeanza na mingine ijiandae.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Agosti 8, 2023) wakati akifunga Kongamano la Vijana katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Ameagiza vijana wapatiwe mbinu na ujuzi wa ujasiriamali ili waweze kuchangamkia fursa zilizopo mbele yao.
Waziri Mkuu amezitaka Taasisi na Mifuko ya Uwezeshaji kwa vijana itangaze fursa zilizopo na watumie mbinu mbalimbali zikiwemo redio hasa za kijamii kuwafikia walengwa. “Kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki katika kuwapa taarifa kuwaongoza na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kukuza mitaji yao.”
“Halmashauri zihakikishe kuwa vijana walio tayari kufanya uwekezaji katika shughuli za uchumi wanapata taarifa za fursa za mitaji. Nyote mlimsikia Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akisisitiza kuhusu kutoa taarifa kwa walengwa.”
Amesema mikoa iandae utaratibu wa kutoa elimu mtambuka kwa vijana ili wapate stadi za maisha na kufanya maamuzi sahihi, masuala hayo ni pamoja na utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI, maadili, uzalendo, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na rushwa.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema vijana wote walioshiriki katika kongamano hilo anaamini wameshaiva na wako tayari kwa kazi, hivyo watumie maarifa waliyoyapata kuchangamkia fursa ziliopo ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma. Vilevile, muwe wadadisi kubaini na kuchangamkia fursa hizo.
”Mmeshapata maarifa mengi kupita kongamano hili wakati umefika sasa mnakwenda kutumia maarifa hayo kwa vitendo. Mikoa nayo iandae utaratibu wa kutoa elimu kuhusu masuala muhimu na mahsusi ya mtambuka kwa vijana ili wapate stadi za maisha na kufanya maamuzi sahihi.”
“Nitoe wito kwenu vijana kuitumia fursa hii muhimu na adhimu mliyoipata katika kongamano hili kuanzisha na kuendeleza miradi yenu na baadaye kuondoa tatizo la ajira na umaskini kwa nchi yetu. Muhimu ni kuthubutu, kuchukua hatua, kuanza kidogo na kukua. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira njema kuhusu ustawi wa vijana.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema kongamano hilo la siku mbili limeshirikisha vijana zaidi ya 3,000 kutoka wilaya zote za mkoa wa Dodoma limelenga kuwawezesha vijana hao kutambua fursa za kiuchumi zilizoko na kuzichangamkia.