Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
SERIKALI inatarajia kuokoa shilingi bilioni 33 inayotumia kuagiza mpira wa mikono (Groves) nje ya nchi baada kukamilisha miundombinu ya kiwanda cha bidhaa hiyo kilichopo Idofi mkoani Njombe na kuanza uzalishaji ndani ya mwaka huu wa fedha.
Meneja Mpango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Bohari ya Dawa (MSD), Hassan Ibrahim, amesema hayo leo Agosti 7,2023 Jijini hapa na kueleza kuwa kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha takribani jozi 86,400,000 za mipira ya mikono kwa mwaka.
“MSD ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miundombinu ya kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi mkoani Njombe na kuanza uzalishaji ndani ya mwaka huu wa fedha.Uzalishaji huu utapunguza utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi na kuokoa sh. bilioni 33 zinazotumika kununua bidhaa hiyo kwa mwaka,”amesema
Ibrahim amesema katika mwaka wa fedha uliopita serikali ilitoa sh. bilioni 157.5 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya.
Amesema hadi kufikia Juni mwaka huu MSD ilikuwa inahudumia jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 7,662 nchi nzima kupitia Kanda zake 10 zilizopo Mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.
“ Idadi hii ya vituo 7,662 ni ongezeko la vituo 597 kutoka mwaka wa fedha 2021/22 ambapo kulikuwa na vituo 7,095,”amesema
Ameeleza kuwa ili kuendana na kasi ya ongezeko la vituo vya afya inayofanywa na serikali ya Awamu ya Sita, Bohari ya Dawa imekuwa ikifanya mawasiliano na balozi ili kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu.
“MSD inapitia mifumo yote ya utendaji na uendeshaji ikiwamo maboresho ya mnyororo wa ugavi, usimamizi wa utendaji na mifumo ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya ongezeko la ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyojengwa na serikali,”amesema
Kuhusu mikakati ya MSD amesema katika mwaka huu wa fedha inatarajia
kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuboresho matumizi ya takwimu za maoteo, kuhakikisha bidhaa zote za afya zinakuwa na mikataba ya muda mrefu.
Amesema pia wamepanga kufanya ugatuzi wa majukumu yaliyokuwepo makao makuu na kuyapeleka katika Kanda ili kuboresha utendaji.