Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amekiri kuvutiwa na uwezeshaji kwa wabunifu wazawa unaofanywa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), aliyoitaka kuhakikisha inaenda mbali zaidi kwa kukifanyia kazi kilio chao cha kutaka kuwapatia Mafunzo ya Mifumo ya Kielektroniki, Ili kuwaongezea ufanisi katika bunifu zao.
Dk. Mpango ameyasema hayo Jumanne ya Agosti 1, alipotembelea Banda la COSTECH, wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane (Tanzania International Agricultural Trade Show 2023), kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, ambako alikuwa mgeni rasmi na kuyazindua kwa kuitaka Wizara na mamlaka husika kutoa tuzo na zawadi za fedha kwa wabunifu wazawa
Akiwa COSTECH, Dk Mpango alivutiwa zaidi na mbunifu Adam Kinyekile ‘Street Engineer,’ aliyewezeshwa na tume hiyo kubuni Mashine Maalum ya kuchakata mazao, ikiwemo kupukuchua nafaka, kusaga nafaka zisizo na mafuta, kuvuta maji ya kumwagilia mazao na kuyabeba mazao hayo baada ya kuvunwa mashambani kupeleka ghalani, ambapo alipokuwa akitoa hotuba ya jumla ya uzinduzi rasmi mbele ya wahudhuriaji, alirudia kuimwagia sifa COSTECH, kwa uwezeshaji kwa kijana huyo na wenzake.
Dk. Mpango aliipongeza COSTECH kwa kuthamini bunifu za vijana wa Kitanzania, ambako alishuhudia bandani hapo bidhaa za Kilimo, Ufugaji na Ufundi kutoka kwa vijana walioshiriki Mafunzo Atamizi, kisha akasikiliza kero na changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi, huku akiitaka tume hiyo kuwaongezea vijana wabunifu Mafunzo ya Kielektroniki, kama alivyoomba Kinyekile Ili kuongeza ufanisi wa bunifu zao, kwani liko ndani ya uwezo wao.
Akizungumzia ubunifu wa Mashine hiyo, Dk. Mpango alimpongeza Adam kwa ubunifu huo, lakini akamshauri kutenganisha kazi za mashine zitokanazo na ubunifu wake Ili kupunguza gharama yake ambayo inaweza kuwa ghali kwa mkulima wa kawaida kuimudu na kubainisha kuwa itakapotenganishwa na kila moja ikafanya kazi tofauti, zitashuka bei na kuwapunguzia mzigo wakulima.
“Kwanza nikupongeze kwa ubunifu huu, tunahitaji vijana wa Kitanzania wabunifu kama wewe. Nitumie fursa hii kuwaomba vijana wote wabunifu wenye uwezo wa kutengeneza Mashine za kuchakata mazao kama hizi wafanye hivyo, COSTECH ipo hapa kwa ajili ya kuwasaidia kama walivyokusaidia wewe na vijana wenzako.
“Mamilioni uliyopewa na COSTECH ni mengi, sio haba kwa mkulima kuyamudu, kwahiyo nashauri utenganishe mashine hizi Ili kupunguza gharama kwa mnunuzi ambaye ni mkulima,” alisema Dk. Mpango na kuitaka tume hiyo kuwasaidia wabunifu hao Ili kubuni mashine tofauti tofauti zinazotumia Mifumo ya Kielektroniki kama alivyoomba Adam.
Awali, Afisa Uratibu na Utafiti wa COSTECH, Dk. Deogracious Protas, alimueleza Makamu wa Rais kuwa, licha ya Sh. Mil. 99 walizotoa kwa Adam, tume yake imesaidia Mafunzo Atamizi ya vijana wanaojihusisha na Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, sambamba na kutoa mitambo yenye thamani ya Sh. Mil. 400 kuboresha usindikaji kwa Kituo cha Utafiti cha TARI Makutupola kilicho chini ya JKT Makutupola, ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa zabibu inayosindikwa hapo kuzalisha mvinyo bora.
Dk. Protas alimuahidi Makamu wa Rais kuwa tume yake italifanyia kazi agizo lake la kutaka iwasaidie wabunifu wazawa kupata Mafunzo ya Kielektroniki Ili kuwawezesha kubuni kwa faida bidhaa zenye mifumo hiyo kwa ustawi wa wakulima na Sekta ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kwa ujumla, Ili iweze kutoa mchango kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza mchango wa Sekta hiyo katika kukuza Pato la Taifa.