Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC), kimesema kiko katika hatua za mwisho za kuweka mfumo utakaowawezesha wawekezaji kupata huduma za mahala pamoja kwa njia ya kielektroniki utakaojulikana kama Tanzania Investment Electronic Window.

Kukamilika kwa mfumo huo kutawawezesha wawekezaji kusajili miradi yao au kupata vibali mbalimbali vya uwekezaji kwenye nyanja mbalimbali wakiwa sehemu yoyote duniani.

Hayo yalisemwa na Ofisa Uwekezaji wa TIC, Elizabeth Muzo,wakati akizungumza kwenye kongamano fupi la uwekezaji lililoandaliwa na taasisi ya Afrika India Business Organization (AIBO).

“Hili dirisha la kielektroniki litakuwa limebeba taasisi 12 za serikali ambazo zinashughulika na kutoa vibali mbalimbali watakuwa wanapatikana wote sehemu moja kwa njia ya mtandao kwa hiyo mwekezaji popote alipo duniani atafungua akaunti yetu ataomba leseni au kitu kingine kwa kutumia mtandao,” amesema.

Kadhalika, amewaaambia kuwa Tanzania bado inahitaji wawekezaji wengi watakaowekeza kwenye mashamba ya kilimo cha miwa ambayo hutumika kuzalisha sukari kwenye viwanda vya ndani.

Amesema wanahitajika pia wawekezaji wa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya kuzalisha sukari kwani soko la bidhaa hiyo bado ni kubwa kutokana na Tanzania kutojitosheleza kwenye bidhaa hiyo.

“Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo inastawi mazao mengi kwa hiyo mkija kuwekeza mtapewa ardhi ya kulima au kuwekeza viwanda kwa muda mrefu na kuna soko kubwa,” amesema,

Alisema serikali bado inaendelea pia kuvutiwa uwekezaji kwenye maeneo ya utafutaji na uchimbaji wa madini kwani utafiti unaonyesha kuwa bado kuna maeneo mengi nchini yenye madini ya aina mbalimbali ambayo hayajachimbwa.

Elizabeth amewaambia wawekezaji hao kuwa kuna fursa mbalimbali na faida ambazo wawekezaji wanapata iwapo watasajili miradi yao kwenye kituo hicho cha uwekezaji ikiwemo kupata msamaha wa kodi kwenye bidhaa mtaji.

Alisema maeneo mengine yenye fursa za uwekezaji ni ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba kwani vifaa na dawa nyingi bado zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

“Maeneo mengine ni ujenzi wa majengo ya kupangisha kwani mahitaji ya majengo ya kupangisha nayo bado ni makubwa kwa hapa nchini kutokana na idadi kubwa ya wawekezaji wanaomiminika Tanzania,” amesema.

Mkurugenzi wa AIBO, Indrabhuwan Singh, alisema kazi ya taasisi yake ni kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji wa mataifa ya Afrika na India kwa kuwaonyesha fursa zilizoko kwenye mataifa hayo na namna wanavyoweza kuzitumia.

“Tunahamasisha usawa kwenye biashara kwa kuwakuza wajasiramali wadogo ili wawe wakubwa na kuiwezesha jamii maskini kupiga hatua kiuchumi kwa namna mbalimbali na tunapigania kuwepo kwa sera nzuri za biashara ambazo zitawezesha ukuaji wa uchumi,” alisema

Aidha, amesema wamekuwa wakifanyakazi kama daraja baina ya wazalishaji na watumiaji kuhakikisha faida inayotokana na biashara watu wote .

Amesema moja ya majukumu ya AIBO ni kuwakutanisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa India na mataifa ya Afrika na kubainisha changamoto za kibiashara zilizopo na kutafuta njia ya kuziondoa ili kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na baishara kwenye mataifa hayo.