Na Albano Midelo, JamhuriMedia,Songea

Mkoa wa Ruvuma unatarajia kuzindua wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama Duniani,Agosti Mosi,2023 katika Kituo cha Afya kata ya Ruvuma kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki amesema Tanzania inaungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama ambayo itaanza Agosti Mosi hadi 7 mwaka huu.

“Lengo la kuhamasisha unyonyeshaji maziwa ya mama ni kulinda na kuendeleza afua ya unyonyeshaji kama njia mojawapo ya kuboresha hali ya lishe kwa watoto’’,amesisitiza Ndaki.

Hata hivyo amesema kwa mwaka huu wiki ya unyonyeshaji maziwa katika Mkoa wa Ruvuma,itafanyika katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma ambapo ametoa rai kwa viongozi,watendaji na wananchi kushiriki kikamilifu kwenye maadhimisho hayo .

Kaulimbiu ya mwaka huu ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama inasema “Saidia unyonyeshaji,wezesha wazazi kulea Watoto na kufanya kazi zao kila siku’’.

Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe unalenga kuweka mazingira rafiki yanayomwezesha mwanamke kunyonyesha ili kulinda na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama.

Kupitia mpango huo serikali na wadau wengine hufanya kazi pamoja kuendeleza, kuhamasisha na kulinda unyonyeshaji watoto maziwa ya mama ili kuimarisha afya ya jamii.

Mpango Jumuishi wa taifa wa Lishe unatambua kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni jukumu la pamoja linaloenda sanjari na utekelezaji wa sera mbalimbali za nchi zinazosaidia kuboresha afya ya mtoto na jamii kwa ujumla.

Please follow and like us:
Pin Share