Na Mwandishi Wetu ,JamhuriMedia, Mwanza

Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa gati na miundombinu muhimu katika bandari za Kibirizi na Ujiji mkoani Kigoma ili kuongeza ufanisi na kuvutia wasafirishaji wengi kutumia bandari hizo zinazotoa huduma katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, na Zambia.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua maendeleo ya miradi hiyo na kuwataka wakandarasi wanaojenga bandari hizo kuongeza kasi ili zikamilike ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari za Ziwa Tanganyika Prof. Mbarawa amesema uwekezaji unaokusudiwa kufanywa katika bandari nchini unatarajiwa kuongeza mapato, ajira na kukuza ufanisi wa utendaji.

“Bandari lazima ziongozwe na kuendeshwa kimkakati kwa kuweka wawekezaji wenye mtandao mkubwa duniani na wenye kumiliki meli nyingi ili kuleta tija“, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa gati la Kibirizi lenye urefu wa takribani mita 259 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 80. Mkoani Kigoma

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Mhandisi Juma Kijavara amesema zaidi ya shilingi bilioni 32.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa gati na miundombinu ya bandari za Kibirizi na Ujiji ikiwa ni muendelezo wa maboresho ya bandari za Ziwa Tanganyika baada ya kukamilika kwa bandari ya Karema Mkoani Katavi.

“Tunaishukuru Serikali kwa namna inavyotoa kipaumbele katika ujenzi wa bandari za Ziwa Tanganyika lengo likiwa ni kuhakikisha zinatumik kikamilifu na hivyo kukidhi soko kubwa la biashara lililopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika na nchi za DRC, Burundi na Zambia.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bw, Salum Kali ameishukuru Wizara ya ujenzi na Uchukuzi kwa namna inavyoshughulikia ujenzi wa miundombinu ya usafiri katika mkoa wa Kigoma na kuwataka wananchi kutumia fursa hizo kufanya biashara na kukuza uchumi.

Zaidi ya boti 18 hadi 20 zitaweza kuhudumiwa kwa wakati mmoja mara ujenzi wa gati katika bandari ya Kibirizi utakapokamilika na hivyo kuvutiawafanyabiashara wengi wa boti mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa gati la Ujiji, Mkoani Kigoma.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa gati la Ujiji ambalo ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 80 na linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, Mkoani Kigoma.