Na Wilson Malima JAMHURI MEDIA, Dar Es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amekitaka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kutilia mkazo masomo yaliyojikita katika utatuzi wa changamoto na tafiti zenye mwelekeo wa kutoa matokeo ili kuweza kupambana na matishio yanayoukabili ulimwengu.

Amesema matishio hayo ni pamoja na itikadi kali, uhalifu wa kimtandao, ukosefu wa ajira kwa vijana, ugaidi, kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya binaadamu, na mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Mpango ameyasema hayo leo Julai 29, 2023 katika mahafali ya kozi ya 11 ya heshima (Valedictory) yaliyofanyika katika chuo cha NDC Kunduchi, Dar es Salaam.

“Hata hivyo sera hii ya mlango wazi inahitaji NDC kudumisha viwango vya juu ili kukidhi matarajio ya kitaifa ya kikanda na kimataifa, ambayo ni kuzalisha wafanyakazi mahiri wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Watumishi wa Umma wenye ujuzi na weledi wa hali ya juu ili kukabiliana na changamoto za ulinzi na kiusalama katika karne hii ya 21.” Amesema Dkt. Mpango

Katika mahafali hayo ya 11 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, jumla ya wahitimu 47 wamekamilisha Kozi zao kwa mwaka 2023 katika ngazi za Umahiri, na Astashahada ya Usalama na masomo ya kimkakati wengi wao wakiwa ni maafisa wa juu wa Majeshi ya ulinzi ya Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa(SADC) na kutoka Bangladesh, India, Nigeria, Misri na Jamhuri ya watu wa China.

Naye Kamanda Mkuu wa Chuo hicho Michael Mhona amesema, ongezeko la machafuko na vita baridi Duniani vimesababisha kubadilika kwa mifumo ya kiusalama kutoka kwa taifa hadi kwa mtu mmoja mmoja na ndiyo maana chuo hicho kinatoa elimu inayowawezesha Maafisa hao kufikiri kimkakati zaidi.

“Kama tunavyojua uwepo ya vita baridi umebadilisha hali ya usalama kwa kiasi kikubwa kutoka kwa serikali hadi watu wanaozingatia usalama hususani wa kibinadamu”.Amesema Michael Mhona

Mabadiliko haya yanahitaji fikra mpya na upendeleo wa usalama. Hii ni kwa sababu vitisho vingi vya usalama vya kisasa katika eneo letu la nchi Afrika na ulimwengu kwa ujumla haviamuru silaha za vita lakini badala yake ni mawindo.amesema na Kuongeza;

“Kwa maana hiyo changamoto za kiusalama tunazokabiliana nazo leo zinahitaji fikra makini na maamuzi ya kina hivyo ndivyo NDC inafanya” Amesema.