Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi wa Shirika la uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)Kaimu Abdi Mkeyenge amesema
katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Juni, 2023 TASAC imeendelea kuimarisha udhibiti huduma za usafiri majini na kuhakikisha kuna ushindani sawia miongoni mwa watoa huduma .

Ameeleza hayo leo Julai 27,2023 Jijini hapa wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo na kusisitiza kuwa kazi kubwa inayofanywa ni kutekeleza ufuatiliaji, tathmini na kutoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa vigezo na viwango vya ubora wa huduma kwa watoa huduma za bandari na usafiri majini.

Mkurugenzi huyo ametaja majukumu ya TASAC kuwa ni kuratibu maombi ya tozo za usafiri wa meli katika Maziwa (Victoria na Nyasa) na kuhakikisha viwango vya tozo vinavyotumika haviathiri ushindani wa kibiashara na kuendelea na zoezi la urasimishaji wa bandari bubu Tanzania bara.

Amezitaja bandari hizo bubu kuwa ni 13 ambazo zimewasilishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa ajili ya urasimishaji na kwamba zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini ya kina kwa kushirikiana na TPA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambapo bandari bubu kumi zilionekana kukidhi vigezo hivyo na kupendekezwa kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) (WUU-U) kwa ajili ya kurasimishwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha waendeshaji wa zilizokuwa bandari bubu binafsi tano za Mwanza ambazo ni miongoni mwa zilizokuwa bandari bubu 20 zilizorasimishwa kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 293/2022 na kupewa leseni za uendeshaji huku TPA wakielekezwa kusimamia kwa karibu bandari kumi na tano (15) zilizobakia.

Katika kutimiza malengo ya kimkakati amesema Shirika limeendelea kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini kwa kufanya ukaguzi wa meli kubwa na vyombo vidogo vya majini na kufanya kaguzi za usalama kwa meli kubwa zibebazo tani 50 au zaidi ili kuhakikisha kuwa ni salama na zinaendeshwa na mabaharia wenye sifa.

“Tuna mabaharia Wenye sifa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza, Kagera, Kigoma na Mbeya ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Juni, 2023, Shirika lilifanya jumla ya kaguzi za meli kubwa 288 ambapo kaguzi 165 zilikuwa za meli za kigeni na kaguzi 123 zilikuwa meli za ndani,”amesema

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameeleza kuwa Serikali inataka kushirikiana na sekta binafsi kuendesha Bandari, mikataba na watakaoendesha bado haijasainiwa.

Amesema,”Sasa hivi ndio wataalamu wako mezani kuzungumza kuhusu mikataba, muda na gharama,lakini hakuna Bandari iliyouzwa, wataalamu watakapokamilisha majadiliano tutaangalia maslahi yetu yako wapi na maoni yanayotolewa na Watanzania yatazingatia,tupo macho wakati wote kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa,”amesema Msigwa.

Please follow and like us:
Pin Share