Wanajeshi katika nchi ya Afrika Magharibi ya Niger wametangaza mapinduzi kwenye televisheni ya taifa.
Walisema wamevunja katiba,wamesimamisha taasisi zote na kufunga mipaka ya taifa.
Rais wa Niger Mohamed Bazoum amekuwa akishikiliwa na wanajeshi kutoka kwa kikosi cha walinzi wa rais tangu mapema Jumatano.
Aliahidiwa “uungwaji mkono usioyumba” wa Washington kwa simu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alisema amezungumza na rais na kumpa uungaji mkono kamili wa Umoja wa Mataifa.
Bazoum ni mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika Afrika Magharibi.
Nchi mbili jirani, Mali na Burkina Faso, zimekumbwa na mapinduzi yaliyochochewa na maasi ya makundi ya Jihadi katika miaka ya hivi karibuni.
Katika nchi zote mbili viongozi wapya wa kijeshi wametofautiana na Ufaransa, koloni la zamani, ambalo pia liliitawala Niger.
Katika tangazo la TV siku ya Jumatano, Kanali Maj Amadou Abdramane, pamoja na askari wengine tisa waliovalia sare nyuma yake, walisema: “Sisi, vikosi vya ulinzi na usalama… tumeamua kukomesha utawala unaoujua.
“Hii inafuatia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama, na utawala mbovu wa kiuchumi na kijamii.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ametoa wito wa kuachiwa mara moja kwa Rais Bazoum.
Blinken amesema wanalaani matukio yanayoendelea Niger ya kunyakua madaraka kwa kutumia nguvu, ambayo yanaivuruga katiba ya nchi hiyo, pamoja na kudhoofisha utendaji kazi wa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.