Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Wazir wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Dkt. Selemani Jafo ameonesha kuridhishwa na uzingatiaji wa Kanuni na Sheria ya Mazingira katika Bandari ya Mtwara.
Hayo yalijiri wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Jafo ya kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira eneo la utunzaji na usafirishaji wa makaa ya mawe zinazofanyika katika bandari hiyo.
Aliupongeza uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mkoani humo kwa kushirikiana na Kampuni ya Ruvuma Coal kwa hatua ya kulinda mazingira.
Aidha, Waziri Jafo amesema ameridhishwa na namna ambavyo wameweka uzio kuzunguka eneo yanapohifadhiwa makaa ya mawe ili kudhibiti vumbi lisisambae na kuathiri wananchi.
“Binafsi nikiwa na dhamana ya kusimamia sekta ya mazingira nimeridhika kwani mmetekeleza maelekezo yangu niliyoyatoa nilipofanya ziara katika siku zilizopita,” amesema Dkt. Jafo.
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amewaelekeza wasafirishaji wa makaa ya mawe kuhakikisha malori yanayosafirisha bidhaa hiyo yanafunikwa kwa turubai ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Akiwa katika eneo la kuhifadhia makaa ya mawe ya Kampuni ya Jitegemee Holdings, alisema ni lazima malori yote yafunikwe kwa kutofanya hivyo kunasababisha vumbi katika mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu biashara.
Pia, amshukuru kwa kuruhusu Bandari ya Mtwara kutumika kusafirishia bidhaa ya makaa hayo yam awe akisema kuwa inaliingizia taifa kipato na kukuza uchumi.
Kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Waziri Jafo, Ahmed ameahidi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ofisi yake kuwasimamia wawekezaji ili kuwa na biashara isiyo na madhara kwa wananchi.
Nae Meneja Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini Mhandisi Boniphace Guni ameahidi kusimamia agizo hilo ili liweze kutekelezeka kwa muda uliopangwa wakati Meneja wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Jitegemee Bw. Boscow Mabena ameahidi kuwa watafuata ushauri wa wataalamu ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Itakumbukwa Desemba 20,2021 Waziri Jafo alipofanya ziara bandarini hapo alitoa muda wa miezi sita kwa uongozi kufanya marekebisho ya dosari za kimazingira zilizobainika ikiwemo kuandaa eneo maalumu lililokidhi vigezo litakalotumika kuhifadhi makaa ya mawe yanayosafirishwa.