*Baadhi ya madereva, makondakta ni miungu watu

Usafiri wa daladala katika Jiji la Dar es Salaam siku hizi ni mithili ya mfupa unaoelekea kumshinda fisi. Baadhi ya madereva na makondakta ni miungu watu! Sijui wanakula pamoja na askari wa usalama barabarani (trafiki)?

Ninasisitiza maneno haya: Baadhi ya madereva na makondakta ni mithili ya miungu watu – wanafanya watakavyo, hawafuati sheria na taratibu zilizopo katika kuendesha biashara ya usafirishaji. Wananchi tunaotegemea usafiri huo, tunalia kwa unyanyasaji mkubwa tunaofanyiwa na baadhi ya madereva na makondakta wa daladala jijini Dar es Salaam kwa kitambo sasa.

 

Ninaposema tatizo hilo linaendelea kukua kwa kasi ya kutisha, si kwamba trafiki hawapo jijini Dar es Salaam, la hasha! Wapo wengi tu lakini ni kama wako likizo vile!

 

Baadhi ya madereva na makondakta wa daladala jijini wamekuwa na  kiburi kupindukia. Wanakatisha safari, wanakataa kwa makusudi kupakia abiria katika baadhi ya vituo. Wanaegesha daladala vibaya kuzuia nyingine kuingia vituoni, hali inayozuia magari mengine kuendelea na safari katika barabara za jirani.


Daladala nyingine zinashusha abiria nje ya vituo, hususan Ubungo na kurudi yatokako, hivyo kukwepa kulipa ushuru unaotozwa na mawakala wa Manispaa kwa kila daladala inayoingia kituoni. Wakati mwingine baadhi ya makondakta wanawatoza abiria nauli kubwa kuliko zilizohalalishwa kisheria na kuandikwa ubavuni mwa daladala zao!

 

Daladala zinazohusika ni pamoja na zinazofanya safari kati ya Ubungo na Posta, Ubungo-Mwenge, Ubungo-Masaki, Mbezi-Posta, Mwenge-Kivukoni, Ubungo-Kariakoo, Buguruni-Kivukoni, Ubungo-Muhimbili, Makumbusho-Posta, Mwenge-Kariakoo, Buguruni-Posta, Mwenge-Temeke, Kimara-Ubungo, Gongo la Mboto-Posta, Ubungo-Kawe, Ubungo-Msasani, Mabibo-Posta, Ubungo-Buguruni, miongoni mwa nyingine nyingi.


Waliokithiri kwa tabia ya kukataa kwa makusudi kupakia abiria katika vituo vya Ubungo na Posta ni baadhi ya madereva na makondakta wa daladala za Ubungo-Mwenge, Ubungo-Posta, Ubungo-Masaki na Mwenge-Posta.


Badala yake wanaondoka na daladala tupu kwenda kupakia abiria katika vituo vya Ubungo Terminal, Manzese na Magomeni. Lengo lao ni kukwepa kupakia abiria kutoka mwanzo (kituo cha daladala cha Ubungo) hadi mwisho wa safari (vituo vya Posta, Masaki na Mwenge). Kero hiyo inashamiri zaidi kati ya saa 1:30 na saa 4:00 asubuhi. Mara nyingi tunashuhudia pia daladala za Posta-Mbezi na Posta-Kimara zinavyoshusha abiria katikati ya safari katika vituo vya Magomeni, Mwembechai, Manzese, Big Brother na Ubungo kinyume cha sheria na taratibu. Trafiki wapo, wanaziona na kuziongoza bila kuzichukulia hatua!


Lakini pia baadhi ya madereva na makondakta wa daladala, hususan za Mwenge-Posta, Kariakoo-Ubungo, Kariakoo-Mwenge na Posta-Ubungo, wakati mwingine huvunja sheria kwa kutoza nauli ya Sh 1, 000 badala ya Sh 300 kwa kila abiria kutoka Posta kwenda Mwenge, Posta kwenda Ubungo, Kariakoo kwenda Ubungo na Mwenge, hususan kati ya saa 1:00 na saa 2:00 usiku, wakati wa msongamano mkubwa wa abiria na magari. Hapa napo hatuwezi kuamini kuwa trafiki hawajui tatizo hili. Hata hivyo, wapo madereva na makondakta wachache wanaotii na kufuata sheria, taratibu na kuongeza ubinadamu katika uendeshaji ya biashara hiyo ya usafirishaji. Hawa ni mfano mzuri wa kuigwa katika jamii.


Katika hali ya kero nilizozitaja na nyingi ambazo sikuzitaja, hivi kweli kuna mtu anayeweza kututafsiri vibaya tunaosema kwamba trafiki, madereva na makondakta ‘wanakula pamoja?’ Kama kuna mtu wa aina hiyo, basi atakuwa na lake jambo. Ninasema hivyo kwa sababu madereva na makondakta wenye tabia hiyo hawafanyi vitendo hivyo vya udhalimu mafichoni katika giza nene, la hasha! Wanavifanya sehemu za wazi mchana kweupe na mbele ya taa zenye mwanga mkali katikati ya Jiji la Dar es Salaam.


Vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na madereva na makondakta wa daladala dhidi ya abiria jijini, vinashawishi wengi kuamini kuwa trafiki waliopo wamefumbwa macho, hawaoni ingawa wana macho, na wamenyamazishwa, hawachukui hatua ingawa wana uwezo wa kuwachukulia wahusika hatua za kisheria.


Kwa upande mwingine, abiria nao hawawezi kukwepa lawama za kuchangia mwendelezo wa karaha zinazowakumba katika usafiri wa daladala, kutokana na kukosa umoja katika kupinga ukiukwaji huo wa sheria. Wengi hawana ujasiri wa kukataa kushushwa katikati ya safari na hawana uthubutu wa kukataa kutozwa nauli kubwa zaidi ya zilizohalalishwa kisheria.

 

Uwezekando wa abiria kuingia na kukataa kulipa nauli kubwa zaidi ya zilizohalalishwa na mamlaka husika upo. Uwezekano wa kukataa kushushwa kabla ya mwisho wa safari zao upo. Lakini ni abiria wangapi wenye ujasiri huo? Ni abiria wangapi wanaoweza kuungana na wachache kutetea haki zao kisheria? Majibu ya maswali haya ni magumu kwa sasa.

 

Binafsi ninaamini kwamba mamlaka zinazostahili kulaumiwa sana kutokana na unyanyasaji unaofanywa na madereva na makondakta wa daladala dhidi ya abiria, ni trafiki na Serikali kwa jumla. Abiria wanaopata mateso hayo wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa letu.


Wamo wanaofanya kazi katika ofisi mbalimbali za umma zikiwamo hospitali, shule, wizara na benki. Ni jambo la fedheha kuona Serikali inawaacha waendelee kunyanyaswa na madereva na makondakta wachache wa daladala wanaokiuka sheria waziwazi.

Uzito wa kero hiyo unaisukuma Fikra ya Hekima kuzikumbusha mamlaka husika, na hasa Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na Serikali kwa jumla, kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva na makondakta wa aina hiyo, kupunguza karaha na kukomesha vitendo vya unyanyapaa dhidi ya abiria.