Na Mwandudhi Wetu, JamhuriMedia, Arusha 

Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Karatu mkoani Arusha, Pamphili Nada, ameuwa kwa kupigwa na kitu kizito na mtu anayesadikiwa kuwa na matatizo ya  akili ambaye alilazimisha kuingia kanisani kwa madai ya kutaka kusali.

Hata hivyo baada ya mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Romani Leonard (30), kufanya mauaji hayo, nae akauawa na wananchi wenye hasira kali.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo.

“Padri alifariki wakati anapelekwa hospitali na mtuhumiwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kupata taarifa za tukio hilo,” amesema.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wakazi wa Karatu wamesema mtu huyo, alikuwa akilazimisha kuingia kanisani kusali tangu usiku wa kuamkia leo, hata hivyo hakufanikiwa baada ya walinzi kumzuia.

Mmoja wa wakazi hao Rehema Baha amesema hata hivyo ilipofika alfajiri mtu huyo aliendelea kupiga kelele kutaka kuingia kusali na ndipo Padri Nada alitoka nje na kumwambia mlinzi amfungulie mlango.

“Baada ya kuingia ndani (kanisani) na akiwa na Padri tu, ndipo alichukuwa chuma cha mlango na kumpiga Padri ambaye alifariki akikimbizwa hospitali,” amesema.

Peter Yohana anasema kutokana na tukio hilo kengere la kanisa ilipigwa na wananchi kukusanyika na baada ya kupata taarifa hizo walianza kumpiga mtu huyo na kusababisha kifo chake.

“Tunamfahamu huyu mtu anatoka Kijiji Gekum Rambo na amekuwa Karatu kwa muda sasa,” amedai

Taarifa zaidi tutawaletea baadaye!

Please follow and like us:
Pin Share