WAZIRI wa Madini ,Dkt Dotto Biteko ametoa rai kwa wazalishaji wa chumvi nchini kuongeza uzalishaji kutoka tani 273,000 hadi tani 303,000 kwa mwaka ili kukidhi soko la ndani na nje.
Rai hiyo aliitoa Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani alipofanya ziara ya siku moja kutembelea na kuona uzalishaji wa chumvi kwenye kampuni za Sea Salt na Stanley and Sons Ltd.
Biteko alieleza, uzalishaji wa chumvi ukiongezeka utasaidia kuongeza mapato na kutoa ajira kwa wananchi ambapo asilimia 15 ya chumvi ndiyo inayopelekwa soko la nje.
“Tanzania ina Pwani kubwa lakini uzalishaji wa chumvi ni mdogo licha ya kuzuia chumvi za nje ili kukuza soko la chumvi inayozalishwa hapa nchini lakini pia wazalishaji wazingatie ubora,”
“Chumvi hiyo inatumika kwa ajili ya chakula, viwandani na kuuzwa soko la nje ambapo chumvi kutoka nje ya nchi inauzwa kwa gharama ndogo ikilinganishwa na inayozalishwa ndani kutokana na gharama za uendeshaji,”aliongeza kusema Biteko.
Alieleza, ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama mamlaka za serikali za mitaa zinapaswa kufanya marejeo ya sheria zake ndogo ili zilingane ambapo kwa sasa kila Halmashauri inatoza gharama zake.
“Serikali baada ya kuona malalamiko ya wazalishaji walifuta kodi 17 na mrabaha kutoka asilimia tatu hadi asilimia moja lengo likiwa ni kupunguza gharama za uzalishaji ili bei iwe ndogo,”alisema Biteko.
Naye Ofisa Madini Mkoa wa Pwani Mhandisi Ally Maganga alisema kuwa Wilaya ya Bagamoyo inazalisha chumvi tani 90,000 hadi 100,000 kwa mwaka na kuingiza kati ya shilingi milioni 300 hadi miluoni 350.
Alieleza, kuna leseni 48 za uchimbaji chumvi huku ndogo zikiwa 46 ambapo ni 15 tu ndizo zinafanya kazi huku nyingine zikiwa hazifanyi kazi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji, soko na mazingira.
Awali Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge alisema, kupunguzwa gharama kwa magari yanayochukua chumvi kutozwa fedha nyingi na Hifadhi za Taifa (Tanapa) ambapo makampuni hayo kutumia barabara za hifadhi ya Saadani.
Mkenge alisema kuwa endapo baadhi ya changamoto zikiondolewa Bagamoyo inaweza kulisha chumvi nchi nzima kwani wanauwezo huo wa uzalishaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya H J Stanley and Sons Richard Stanley alifafanua wanakabiliana na changamoto ya uingizwaji wa chumvi toka nchi nyingine ambapo miundombinu ikiwa mizuri gharama za chumvi zitapungua na bei itashuka.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Shauri Selenda alisema kuwa kilio cha wawekezaji hao kinafanyiwa kazi kwa kuboresha miundombinu na upatikanaji wa maji na umeme na barabara.
Alisema tayari miundombinu hiyo imewekwa kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha ili kuwaondolea kero wawekezaji hao.