Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Serikali imetaja sababu ya Kampuni ya DP World kuja kufanya shughuli za uboreshaji wa bandari hapa nchini.

Hayo yamebainishwa leo Julai 14, 2023 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa wakati akizungumza na Jukawa la Wahariri Tanzania (TEF), jijini Dar es Salaam.

Prof.Mbarawa amesema DP World ina uwezo mkubwa katika uendeshaji wa shughuli za bandari hivyo itachochea mnyororo mzima wa usafirishaji wabidhaa mpaka kwa walaji.

Mbarawa amesema kuwa kampuni hiyo ina uwezo kwani inamiliki meli zaidi ya 400 za mizigo kupitia kampuni yake nyingine, jambo ambalo litaongeza ufanisi mkubwa katika usafirishaji wa mizigo.

“Kampuni nyingine hazikukidhi sifa za mwekezaji mahiri ambaye anahitajika kwani hazikuwa na uwezo wa uchagizaji wa mnyororo mzima wa usafirishaji wa mizigo,” amesema.

Naye Mtaalamu mbobevu wa mikataba ya Kimataifa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usafiri wa Anga na kiongozi wa majadiliano ya Serikali katika suala la majadiliano ya Mkataba wa Bandari, Hamza Johari ametoa ufafanuzi wa vipengele mbalimbali kuhusiana na mkataba huo na kusema kuwa mwekezaji DP World hatomilikishwa ardhi ya Tanzania na badala yake atakodishwa.

Amesema kuwa bado mkataba wa bandari haujasainiwa na kilichopo sasa ni makubaliano ambayo yanajenga msingi wa mkataba ambao utaandaliwa kwa ajili ya kuongoza ushirikiano wa kiuchumi kati ya serikali ya Tanzania na Dubai.

Amesema iwapo mkataba huo ukianza utekelezaji kwenye bandari ya Dar es Salaam, italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa manufaa ya watanzania kupitia mwekezaji DP World.

“Nchi haijauzwa na kwamba mwekezaji DP world atakuwa na asilimia 8 tu katika uendeshaji wa baadhi ya maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam na kusisitiza kuwa DP World bado hajaanza kufanya kazi nchini kama inavyodaiwa na wapotoshaji kuhusu suala la uwekezaji huo,” amesema.

Amesema suala la uwekezaji wa kampuni ya DP World halipo kwenye mambo ya Muungano wa nchi saba zinazounda Umoja wa Falme za Kiarabu, hivyo katiba yao imetoa haki kwa moja ya nchi wanachama kuingia kwenye ushirikiano na nchi yoyote.

Amesema majadiliano hayo tayari yameridhiwa na Bunge ili kuyalinda, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.

Pamoja na mambo mengine, amesema majadiliano hayo yaliyoanza tangu mwaka 2018, yana kipengele kinachowezesha kama mkataba utasainiwa kutakuwa na nafasi ya marekebisho kwa pande zote mbili.