Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi-Dar es Salaam
Jeshi la Polisi limesema kuwa litaendelea kuunga mkono juhudi za Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la ulinzi na usalama Daktari Samia Suluhu hassan Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kukuza utalii na kuongeza watalii Nchini kwa kuimarisha ulinzi na usalama kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Hayo ameyasema mkuu wa kituo cha utafiti cha Jeshi la Polisi kilichopo chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) kamishna msaidizi wa Polisi ACP Ralf Meela katika mafunzo yaliyotolewa na wakufunzi kutoka chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kwa wanafunzi wanaoendelea na kozi mbalimbali chuoni hapo.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuuongeza weledi katika kutoa huduma bora kwa wageni ambao wanafika nchini kwa ajili ya utalii.
Ameongeza kuwa katika kuunga mkono juhudi hizo Jeshi la Polisi nchini limeanzisha kitengo maalum kwa ajili ya kutoa huduma za kitalii na kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia kilichopo jijini Arusha ambacho kinahusika moja kwa moja na kutoa huduma kwa watalii na wanadiplomasia wanapokuwa Nchini.
Kwa upande wake Mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa cha utalii Amiri Abdu amesema kuwa wametoa mafunzo hayo kwa Jeshi la Polisi ambao ndio wadau wakubwa katika maswala ya ulinzi na usalama na amebainisha kuwa Jeshi hilo linanafasi kubwa ya kuongeza idadi ya utali kutokana na kuimarisha ulinzi kwa watalii.
Naye Mwanafunzi wa kozi ya mkaguzi msaidizi wa Polisi Naomi Laizer amebainisha kuwa, wamejifunza na kuelewa vyema dhana ya utalii na mtalii ambapo amesema, mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi wakati taifa linapokea wageni wengi kwa sasa na wameahidi kutoa huduma bora kwa watalii.
Malius Nyenza mwanafunzi wa kozi ya uofisa amebainisha kuwa mafunzo hayo yamewajenga na kuwaongezea maarifa katika sekta hiyo ya utalii ambayo inachangia pato kubwa katika taifa na amesema kuwa, kama Jeshi la Polisi wataendelea na utaratibu wao wa kila siku wa kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao wakiwemo watalii wanaoingia Nchini kwa ajili ya utalii.